FELIX MWAGARA, MOHA – KIBAKWE

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema katika operesheni ya kuwasaka majambazi inayoendelea nchini kati ya majambazi kumi wanaokamatwa mitaani, watatu wanatoka gerezani.

Amesema kuwafunga majambazi hao hakusaidii sana kwasababu wanarudi mitaani na kuendelea kufanya uhalifu wa aina mbalimbali pamoja na kuwaua watu wenye haki, hivyo watatafuta namna nyingine ambayo watamalizana na majambazi hayo.

Waziri Simbachawene amezungumza hayo,  katika Kata ya Pwaga, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, katika ziara yake inayoendelea ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake, ambapo amesema licha ya kuwa wamemalizana na majambazi hayo lakini bado Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni ya kuwasaka itakayo kamilika Julai 28, mwaka huu.

“Ukikamata majambazi kumi, watatu wametoka gerezani, ama kwa msamaha au kwa kumaliza kifungo, wanarudi tena kufanya uhalifu, sasa tutaendelea kuwafunga wanarudi kufanya uhalifu, tunawafunga wanarudi kuua watu wenye haki, hapana, nasisi tutatafuta namna ambayo tutamalizana vizuri,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, “Unapopigania uhai wa watu wenye haki kwa njia yoyote ile wala hautendi dhambi, kwahiyo tutajua namna tutakayomalizana, na mimi nawaambia, Rais Samia alisema siku ile tusibonyezeke, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Rais hatujabonyezeka, walipotubonyeza tuliponyanyuka juu hatukubonyezwa tena,  tumehakikisha mpaka tumeelewana Kiswahili, kwa hiyo tumemalizana tunaenda vizuri, na narudia kusema tena waache waamue kufanya kazi halali.”

Aidha, Waziri Simbachawene alisema wanaohusika na uhalifu ni watu wanaotoka katika jamii, wananchi wanawajua, ili kudhibiti matukio ya uhalifu wananchi hao wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wanaofanya uhalifu huo katika sehemu wanazoishi.

Alisema baadhi ya wahalifu hao wanavamia maduka ya mpesa, tigopesa, airtel money na mengineyo, wanachukua fedha, hatua ambayo inaleta taharuki mitaani.

Waziri huyo aliwataka wananchi wajue kuwa majambazi wanapofanya uvamizi huo katika maduka hayo, wanapaswa kujua wamevamiwa wao hivyo washirikiane ili kupinga hatua hiyo.

“Ndugu zangu ukiona jirani yako au mtu anayewapa huduma hapa kijijini amevamiwa, na nyinyi kijijini kizima mtakuwa mmevamiwa, mtu anaporwa na majambazi wanatumia silaha, lakini nyinyi mnaona kama kitu cha kawaida tu, Wamasai wale akiibiwa mfugaji mmoja ng’ombe wanatoka wote kusaka huyo aliyeiba” alisema.