JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

RAIS Cyril Ramaphosa amesema kuwa hatoruhusu machafuko na ghasia kutawala nchini Afrika Kusini na kudokeza kuwa wimbi la vurugu ambazo ziliharibu mamia ya maduka na kuwauwa zaidi ya watu 100 lilichochewa makusudi.

Akizungumza katika Manispaa ya Ethekwini, ambayo inajumuisha mji wa bandari wa Durban, na ambao ulikuwa mojawapo ya maeneo yaliyoathirika pakubwa, Ramaphosa alisema uporaji huo na uchomaji moto vimeathiri pakubwa imani ya wawekezaji na kuathiri ukuaji uchumi wa Afrika Kusini.

Alifahamisha kuwa serikali yake inafanya kila liwezekanalo kutuliza hali hiyo. Katika taarifa yao kwa kamati ya bunge, polisi ilisema uporaji bado unaendelea na maduka yanayomilikiwa na wageni yanavamiwa.

Mikoa ya Gauteng na KwaZulu-Natal bado ni tete na watu wamekusanyika katika mikoa ya Cape Mashariki, Cape Kaskazini na Cape Magharibi.