ZASPOTI
MENEJA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, amesaini mkataba mpya utakaomuweka na klabu hiyo hadi mwaka 2024, na chaguo la mwaka mmoja zaidi.
Raia huyo wa Norway mwenye umri wa miaka 48, alichukua madaraka kamili mnamo Machi 2019, baada ya kukaimu nafasi hiyo wakati Jose Mourinho, alipotupiwa virago.
Aliiongoza United kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita na fainali ya Ligi ya Uropa, ambayo walipoteza.
Solskjaer, alisema, amefurahia kusaini mkataba huo mpya.
“Tuna imani zaidi ya hapo awali kuwa chini ya uongozi wa Ole, tunaelekea katika muelekeo sahihi”, alisema, makamu mwenyekiti mtendaji wa United, Ed Woodward.
“Ole na wafanyakazi wake wamefanya kazi bila ya kuchoka kuweka misingi ya mafanikio ya muda mrefu uwanjani.
“Matokeo hayo yamezidi kuonekana katika misimu miwili iliyopita na sote tunatarajia kuona timu ya kusisimua ikiendelea zaidi katika miaka ijayo.
“Kinachofurahisha zaidi ni jinsi maendeleo haya yamepatikana na mchanganyiko wa vipaji vijana, vipaji vya nyumbani na waajiriwa wa kiwango cha juu, wanaocheza mpira wa kushambulia katika mila bora ya Manchester United.”
Solskjaer alitumia misimu 11 kama mchezaji wa United, akifunga goli la ushindi katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.
Amekuwa meneja wa kudumu wa nne wa United tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mnamo 2013 aliposaini kandarasi ya miaka mitatu mnamo Machi 2019.
Solskjaer aliongoza klabu hiyo ya Old Trafford kushika nafasi ya tatu katika msimu wake wa kwanza kamili wakati pia walifikia nusu fainali ya Ligi ya Europa kabla ya kupoteza mbele ya Sevilla.
Katika kampeni iliyopita, United ilimaliza pointi 12 nyuma ya mabingwa Manchester City na ilishika nafasi ya pili huku ikichapwa na Villareal kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya Ligi ya Europa.
Habari ya mkataba mpya wa Solskjaer inafuatia uthibitisho wa klabu hiyo kumsajili winga wa Uingereza, Jadon Sancho kwa pauni milioni 73 kutoka Borussia Dortmund.
“Kila mtu anajua hisia nilizonazo kwa klabu hii”, alisema, Solskjaer.
“Ni wakati wa kufurahisha kwa Manchester United. Tumeunda kikosi kilicho na usawa mzuri wa vijana na wachezaji wazoefu ambao wana njaa ya mafanikio.
“Nina timu nzuri ya ufundi karibu yangu na sisi sote tuko tayari kuchukua hatua inayofuata katika safari yetu.
“Manchester United inataka kushinda mataji makubwa na bora na hiyo ndiyo tunayojitahidi. Tunajiimarisha, ndani na nje ya uwanja, na hilo litaendelea kwa misimu ijayo”.
Sancho amesema kujiunga na Manchester United ni ‘ndoto inayotimia’, akiwa ndiye mchezaji wa pili ghali wa Kiingereza wakati wote nyuma ya mwenzake mpya wa United, Harry Maguire.
Amesajiliwa na United kwa mkataba wa miaka mitano.
“Nitaishukuru Dortmund kila mara kwa kunipa nafasi ya kucheza soka kikosi cha kwanza, ingawa siku zote nilijua kwamba nitarudi England”, alisema, Sancho mwenye umri wa miaka 21.
“Nafasi ya kujiunga na Manchester United ni ndoto iliyotimia na siwezi kungojea kuburudisha kwenye Ligi Kuu England.
“Hiki ni kikosi cha vijana na cha kusisimua na naelewa, kwa pamoja, tunaweza kukuza kitu maalum cha kuleta mafanikio ambayo mashabiki wanastahili.”
United ilikubali ada ya Sancho mnamo Julai 1 na mkataba wake wa miaka mitano na klabu una chaguo la miezi 12 zaidi.
Sancho alifunga magoli 50 na kutoa usaidizi 57 katika mechi 137 za Dortmund. (BBC Sports).