RIYAD, SAUDI ARABIA

SULTAN Haitham Tarik wa Oman amefanya safari ya kwanza nje ya nchi kwa kuitembelea Saudi Arabia, ikiwa pia ni mara ya kwanza kufanywa na kiongozi mkuu wa Oman huko Riyadh baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Sultan Haitham Tarik aliwasili nchini Saudia kwa ziara ya siku mbili kuitikia mwaliko rasmi aliopewa na Mfalme Salman Abdulaziz Aal Saud wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Saudi Arabia SPA, katika uwanja wa ndege, Sultan wa Oman alilakiwa na mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammad Salman pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo akiwemo waziri wa mambo ya ndani na balozi wa Saudia nchini Oman.

Imeelezwa kuwa, ziara hiyo ya Sultan Haitham Tarik nchini Saudi Arabia inalenga kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kupanua wigo wa ushirikiano na njia za

kuustawisha katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya hali bora ya maisha na ustawi wa wananchi wa nchi mbili hizo.

Aidha, mazungumzo ya viongozi wa nchi hizo mbili yameelezwa kuwa ni mwendelezo wa harakati za kidiplomasia zinazofanywa na Sultan wa Oman kwa madhumuni ya kuyapa msukumo mazungumzo ya amani ya Yemen kulingana na mapatano yaliyofikiwa kikanda na kimataifa kwa lengo la kuhitimisha vita vya miaka saba na kuzikutanisha katika mazungumzo ya ana kwa ana pande husika katika vita hivyo.