NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita ameishauri benki ya CRDB katika vipaumbele vyake yasaidie makundi ya wanawake na wajasiriamali ili yakwamuke kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Waziri huyo alieleza hayo wakati alipokuwa akizindua kampeni iliyoandaliwa na benki hiyo iliyopewa jina la ‘Tupo mtaani kwako’ ambayo iko kwenye awamu ya pili, hafla iliyofanyika Michezani Mall.

Alisema wanawake na wajasiriamali ni makundi yanayopambana katika kukabiliana na ugumu wa maisha, hata hivyo tatizo kubwa linaloyakabili makundi hayo ni kupata mikopo ya kuendeleza biashara zao.

Aidha alisema changamoto nyengine inayoyakabili makundi hayo ni taaluma ya kufikia viwango vya juu vya uzalishaji wa bidhaa za kisasa pamoja na masoko changamoto ambazo CRDB inaweza kuzitatua.

Waziri Tabia alisema serikali inakabiliwa na ufinyu wa nafasi za ajira, hivyo kuwezeshwa kwa makundi hadi kumudu kutekeleza majukumu yake kutasaidia kupunguza tatizo hilo na kuifanya sehemu kubwa ya jamii ijitegemee.

“Nakuombeni sana CRDB wasichague mitaa ya kwenda kwani wananchi wanahitaji huduma za kifedha na wizara yetu itaendelea kuwaunga mkono kwa ajili ya kuwainua vijana na wajasiriamali”, alisema waziri huyo.

Sambamba na hayo aliwasisitiza vijana kutumia fursa kwa kufanya kazi ipasavyo ili kusudi kuzalisha shughuli zao za kimaendeleo kwa kujiongezea kipato na kusaidia familia zao.

Aidha aliwataka kinamama kuacha muhali kwa kuwafungulia watoto akaunti za akiba benki kwa ajili ya kuwawekea fedha zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadae.

Kwa upande wake, meneja wa benki ya CRDB Tawi la Zanzibar, Ahmada Abubakar alisema benki hiyo imelenga kutoa elimu ya huduma za kibenki ambazo wanazitekeleza katika maeneo mbalimbali.

Pia alisema benki yao ina lengo la kusaidia wajasiriamali, vijana na watanzania wote ili kuweza kujiunga na kunufaika ambapo kampeni hiyo  itadumu kwa muda wa siku nne.