NA MWANAHAWA HARUNA, SCCM

WAZIRI wa Habari, Vijana, Sanaa na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amempongeza msanii wa Bongo Fleva kutoka kundi la Wasafi, Zuhura Othman (Zuchu) kwa kuamua kuwaunga mkono wasanii wa Zanzibar.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na vyombo vya habari katika hafla iliyoandaliwa na msanii huyo katika hoteli ya Verde Mtoni.

Alisema msanii huyo ameoesha dhamira njema ya kuwasaidia wasanii wa Zanzibar ili kuweza kuwasaidia kufikia malengo yao katika musiki na kuwataka wasanii wa Zenji Fleva kuweza kutumia fursa hiyo.

Alisema dhamira ya msanii huyo imeonesha kuwa mapenzi aliyonayo kwa wasanii wa Zanzibar wa Zenji Fleva wananyanyuka kimuziki na wanakuwa juu kama wasanii wengine.

“Nyote ni mashahidi tunao wasanii wengi Zanzibar ambao wana vipaji vizuri lakini bado kuna mambo ambayo yanawapelekea sanaa yao kutoinuka na kupelekea kupotea na wengine hawajafika pale ambapo wanataka kufika,” alibainisha.

Waziri Tabia aliahidi kuwa wizara yake itaunga mkono katika jambo ambalo lina manufaa makubwa kwa wasanii wa Zanzibar na kuwataka wasanii wa Zenji Fleva kushirikiana na msanii huyo kwani watapata taaluma ya kuimarisha kazi zao, kupata soko na tija kwa kazi zao kwa kuinua vipaji vyao.

“Tumeamua kuwasaidia wasanii wetu wa Zanzibar na pamoja kuuza muziki wa Tanzania hii ni bahati ya dhahabu, tuitumie vizuri naamini kwamba tukifanya hayo tutakwenda katika muziki wa aina nyengine, kubadilika na kupata fursa nyingi wasanii wa Zanzibar,” alibainisha.