NA NASRA MANZI,WHVUM
WAZIRI wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita juzi amewaongoza viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Elimu katika mapokezi ya wanamichezo walioshiriki mashindano ya Umisseta huko Mtwara.
Mapokezi hayo yaliyoanzia bandarini hadi katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil kwa kufanyiwa sherehe ya aina yake.
Akizungumza baada ya kuwapokea wanamichezo hao huko bandari ya Zanzibar Malindi ,waziri huyo alisema serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo itaendelea kuimarisha na kurejesha haiba ya michezo ili kuibua vipaji sambamba na kuipatia sifa Zanzibar katika michezo mbali mbali.
Alisema michezo ndio nembo ya nchi,hivyo ni vyema vijana kutumia michezo na sanaa kwani ndio chachu ya maendeleo katika maisha yao.
Aidha alisema ubingwa walioupata katika michezo mbali mbali ya Umisseta ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi katika kuinua na kuimarisha michezo.
Tabia aliwataka wanamichezo kusoma kwa bidii ili kuwajenga katika michezo kwa lengo la kuibua vipaji vyao.
Aliwapongeza wanamichezo hao kwa jitihada walizozionesha kwani wameitangaza Zanzibar kuwa bado vipaji vipo na vinaendelezwa.
Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Michezo Idara ya Michezo Wizra ya Elimu Mussa Abdulrabi Fadhil, amesema katika kuhakikisha michezo wanaimarisha mwakani ameomba kuongezwa wachezaji kutoka kisiwani Pemba ili kufikia malengo zaidi.
Nae Mratibu Idara ya ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mzee Ali Abdalla ameiomba Wizara ya Elimu kuzidi kusimamia sera ya elimu kupitia Idara ya michezo ili kusudi kuimarisha sekta ya michezo maskulini kwa vitendo na nadharia.
Kwa upande wa wanamichezo hao Kanda ya Unguja na Pemba wameipongeza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Elimu kwa kuwaunga mkono Vijana wao kwani imewapa ari na nguvu ya kuendeleza vipaji vyao.