NA MAULID YUSSUF, WEMA
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamduni na Michezo Tabia Maulid Mwita, amesema , bado juhudi zinahitajika ili kuendeleza vipaji vya wabunifu wa sinema nchini.
Akizungunza wakati wa hafla ya usiku wa zawadi wa Tamasha la Kimataifa la filamu Zanzibar, (Zanzibar International Film Festival), ukumbi wa Ngome kongwe, ambapo hutuba yake ilisomwa kwa niaba na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Simai Mohammed Said.
Alisema kuimarisha tamasha hilo kutasaidia sana kuibua vipaji vya vijana na kuitangaza Zanzibar kiutalii zaidi pamoja na kupelekea jina la Tanzania liendelee kukua nchi za nje.
Aidha alisema akiwa mwenye dhamana ya elimu nchini ata hakikisha anainua vipaji katika skuli mbalimbali, ili kukuza tamasha hilo kwa kuwa na wabunifu wazalendo.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF Hassan Mitawi alisema tamasha hilo, linaleta muamko kwa Wazanzibari katika suala la utunzaji mazingira bila ya kuharibu mila zao.
Alisema tamasha hilo linawakilisha maonesho mbalimbali ambayo yanaelimisha na kuihamasisha jamii juu ya kujilinda na maradhi, kulinda mazingira na kudumisha mila na tamaduni za kizanzibari hali inayopelekea Zanzibar kuzidi kujulikana duniani kote na kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Nae Mkurungenzi wa ZIFF Martin Muhando alisema tamasha la ZIFF linawasilisha utamaduni wa Zanzibar, pamoja na wakaazi wake hasa katika masuala ya utamaduni wao ambapo huwavutia sana wageni wanaokuja kutembelea visiwa vya Zanzibar.
Alisema kutokana na mazingira mazuri na ukarimu wa watu wa Zanzibar imepelekea kuwa na ongezeko la wadhamini na wadau wengi ambapo pia linaongeza furaha na amani kwa wageni na wenyeji wa visiwa vya Zanzibar.
Aidha wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kulisimamia tamasha hilo ili libaki Zanzibar kwani ndio asili ya Tamasha hilo.
Tamasha la 24 la ZIFF limeshirikisha jumla ya filamu 67, ikiwa filamu 11 kati ya hizo zimeonekana kufanya vizuri kwa mwaka huu, ambapo filamu ya RUPIA imeshinda tunzo ya EMARSON kwa mwaka 2021.
Hafla ya usiku wa zawadi ni miongoni mwa shamrashamra za 24 za tamasha la Zanzibar International Film Festival ambazo hufanyika kila mwaka visiwani Zanzibar.