NA NASRA MANZI, WHVUM
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amewataka wanafunzi wa ‘Zanzibar School of Health’, kuendelea kushiriki michezo na kusoma kwa bidii kwani serikali inahitaji wataalamu katika sekta ya afya.
Hayo ameyaeleza katika fainali ya mashindano ya ‘ZSH cup,’ iliyowakutanisha timu ya Madawa dhidi ya timu ya DC mchezo uliopigwa uwanja wa Mao Zedong.
Alisema elimu na michezo ni vitu muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi, hivyo vijana watumie taaluma hizo ili kuzalisha wataalamu kwa lengo la kuisaidia jamii.
“Vijana someni kwa bidii huku mkishiriki michezo katika skuli zenu, kwani serikali inajitahidi kutatua kero za wananchi na imejipanga kuongeza ajira sekta ya afya” alisema
Tabia alisema wataalamu katika sekta ya afya ni muhimu kwani hata katika michezo kumekuwa na wataalamu ambao wanawasaidia vijana kupitia michezo mbali mbali,ili kusudi panapotokea majeruni kusaidiwa.
Aliongeza kuwa Wizara ya Habari ,Vijana, Utamaduni na Michezo itaendelea kushirikiana na vijana katika kuendeleza na kuinua vipaji vyao ili kujipatia fursa mbali mbali za kimichezo.
Mkurugenzi wa Zanzibar School of Health’ iliyopo kwa mchina Aziza Hamid alisema mashindano hayo ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi katika kuibua vipaji na kuimarisha michezo katika skuli zao.