NA NASRA MANZI, WHVUM

WAZIRI wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amewataka wasanii visiwani Zanzibar, kuzingatia vyema utamaduni,mila,maadili na silka za mzanzibari wanapofanya kazi zao.

Hayo ameyaeleza wakati akifungua mafunzo elekezi kwa wasanii tofauti wa Zanzibar yaliyofanyika kwenye ukumbi wa studio za filam na muziki Raha leo Mjini Unguja.

Alisema lengo la mafunzo kuona jinsi gani sanaa na wasanii wa Zanzibar wanapiga hatua katika kuimarisha kazi na kujipatia soko, pamoja  na kulinda maadili yao kwa kutumia fursa na kuyatekeleza kwa vitendo.

Alisema atahakikisha kazi zao zinasambaa kupitia vyombo vya habari,lakini pia aliwataka wasanii hao kujilinda, kujichunga na kufanya kazi vizuri ili serikali  kuwatumia katika shughuli mbali mbali  za kiserikali.

” Tumieni sanaa zenu kwa kushirikiana kulinda maadili na kujichunga na viashiria serikali yenu bado inaitaji vijana imara, lakini kumbukeni   bado Rais Dk. Hussein Mwinyi anawaunga mkono katika kuinua sanaa na kazi zenu mnazozifanya” alisema

Aidha alieleza baadhi ya wasanii wanatumia vibaya kazi zao ikiwemo kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya hivyo, amewataka waache tabia hiyo na badala yake wasanii kuwa mfano wa kupinga utumiaji wa  dawa  hizo katika sanaa zao kwa kufikisha ujumbe kwa jamii.

Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka alisema sanaa ni muhimu na imekuwa na mwamko katika jamii ,hivyo waitumie kwa lengo la kuikuza ambayo itawawezesha wasanii  hao kujitegemea kiuchumi.

Kwa upande wake rais wa wasanii Zanzibar Mohamed Laki amewataka wasanii kushirikiana na kutumia mitandao ya kijamii kwa lengo la kukuza kazi zao Ili kujiletea maendeleo.

Mafunzo  hayo yaliyoandaliwa na msaanii maarufu Zuhura Othman ‘Zuchu’ na uongozi wake ambapo jumla ya wasanii 133 walihudhuria.