NA HASHIM KASSIM
KATIBU mkuu wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wilfred Kidau amesema wako tayari kuendeleza mashirikiano na shirikisho la soka Zanzibar (ZFF), hasa kwa rais mpya aliyechaguliwa hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hili baada ya kikao cha kujadili mashirikiano kilichofanyika katika ukumbi wa baraza la michezo Zanzibar, ameeleza kuwa kuna ushirikiano wa kutosha na ZFF tofauti na inavyoelezwa.
“Ni kikao kizuri na tumekua na mashirikiano mazuri na ZFF tofauti na watu wanavyosema, kwa miaka ya karibuni tumekua tunafanya kazi kwa karibu na TFF ilisaidia kumaliza ligi ya Zanzibar kipindi cha Covid sisi ndio tuliotoa rasilimali fedha kuweza kumalizia” alisema Kidau.
Akiongezea kuwa si hayo tu kuna mengi ambayo hukaa na kushirikiana na ZFF ikiwema masuala ya uendeshaji wa mpira kwani wote wanasimamia soka na lengo ni kuukuza mpira wa Tanzania.
Sambamba na hayo katibu huyo alisema wapo pamoja na ZFF katika kila jambo na wataongeza mashirikiano hayo kwa rais aliyechaguliwa wa shirikisho hilo.