NA WUU

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limesaini mkataba wa ununuzi wa vichwa 17 vya treni ya umeme na jozi 10 za treni ya abiria zitakazotumia umeme yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni sita.

Mkataba huo uliosainiwa baina ya TRC na kampuni ya Hyundai Rotem, kutoka Korea na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho mkoani Dar es Salaam umejumuisha pia na ununuzi wa kifaa cha kufundishia madereva watakaoendesha treni ya kisasa ya SGR mara pindi ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika.

Katika halfa hiyo ya utiaji saini Waziri Dk. Chamuriho, ameagiza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuhakikisha wanatumia wataalam wa ndani katika uendeshaji wa miundombinu ya treni mpya ya reli ya kisasa ya SGR.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huu kuanzia miundombinu yake hadi sasa tunanunua vifaa kwa gharama kubwa hivyo vyema tukawajengea uwezo wataalam wetu waweze kuendesha treni hii ya kisasa”, amesisitiza Chamuriho.

Aidha, amawataka wale ambao watapata fursa ya kuaminiwa kufanya kazi katika treni hizo kufanya kazi kwa weledi kwa ajili ya maslahi ya Taifa.