TUNAPASWA kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa salama dhidi ya janga la maradhi ya corona ambalo kwa sasa linaendelea kuwa tishio kubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine duniani ilikuwa miongoni mwa nchi ambazo baadhi ya watu walithibitika kuambukizwa ugonjwa wa corona mnamo mwezi Machi mwaka 2020.

Ugonjwa huo uliendelea kuishi nchini kwa miezi kadhaa hadi mwezi Juni ya mwaka 2020, ndipo corona ilipopungua na hatimaye kutoweka kwa kutokuwepo maambukizi.

Mnamo mwishoni mwa mwaka 2020 na mwanzoni mwa mwaka 2021, corona ilifumuka upya, hichi ndicho kipindi kilichoitwa wimbi la pili la ugonjwa wa corona.

Hata hivyo msisitizo uliokuwa ukitolewa ni kuhakikisha wananchi wanachukua jitihada za kujikinga na maambukizi mapya na kusisitizwa kutumia tiba za asili.

Lakini alipoingia madarakani Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, moja ya ahadi zake ni kuunda tume maalum ya wataalamu itakayoishauri serikali namna ya kukabiliana na janga hilo.

Kwa sasa tume hiyo imekamilisha jukumu lake na imetoa mapendekezo takribana 19 kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini.

Katika mapendekezo mengi yaliyopendekezwa na kamati hiyo ni tishio la Tanzania kukubwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa corona.

Zipo nchi nyingi kwa wakati huu zinapitia kipindi cha wimbi la tatu la ugonjwa wa corona ikiwemo India ambapo hadi kirusi cha corona kilichogunduliwa nchini humo kinaitwa kirusi cha India.

Hali kama hiyo pia ilikuwepo Afrika Kusini, Brazil, Marekani, Uingereza pamoja na nyengine ambapo wimbi la tatu la ugonjwa huo lilikuwa baya sana kwani maambukizi yalikuwa ya kasi sana na watu wengi wamefariki.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lazima zichukulie kwa makini tishio la kutokewa kwa wimbi la tatu kwa sababu kawaida linakuwa bay asana.

Mbali na serikali zetu, lakini jitihada kubwa katika kujikinga na corona ni jukumu la kila mwananchi hasa ikizingatiwa kuwa njia zote za maambukizi zinajulikana hivyo ni suala la utekelezaji.