WAISLAMU wa Zanzibar leo wanaungana na waislamu wenzao duniani kote kusherekea sikukuu ya Eid al – Adha au kama inavyotambulikana kuwa ni Eid ya kuchinja.

Waislamu husherekea Eid al – Adha, kufuatia waumini wa dini hiyo waliojaaliwa kuitekeleza ibada ya hijja huko katika mji mitakatafu ya Makka na Madina nchini Saudi Arabia kuikamilisha.

Tunaelewa kwa mwaka wa pili mfululizo kumekuwa na idadi ndogo ya waumini wanaoshiriki ibada ya hijja na hilo linatokana na nchi ya Saudi Arabia kuweka karantini ya udhibiti w amaradhi ya corona.

Kwanza kabisa tunapaswa kuwaombea kila la kheri waislamu wenzetu waliojaaliwa kwenda kutekeleza ibada ya hijja na kuimaliza salama wakiwa wazima wa afya.

Aidha ni vyema tuwaombee kwa Mwenyezi Mungu azikubalie dua na ibada zao za hijja, ibada nyengine walizozifanya, awasamehe makosa yao yote na mwisho wa siku awaingize katika pepo yake.

Kwa upande wao mahujaji wetu wapya wanawajibu mkubwa wa kuziombea mema familia, ndugu, jamaa na hata kuiombea nchi yetu ipate baraka na iendelee kuwa na amani na utulivu.

Tunaamini mahujaji wetu mara baada ya kurudi nyumbani watakuwa mabalozi wazuri waliobadilika kwa miendendo na matendo kwa kutekeleza maamuru yote ya dini.

Kwa hakika tunaamini mahujaji wetu wapya watakuwa kioo na kigezo kizuri sana cha jamii na watakuwa msaada mkubwa katika kuisaidia jamii kuishi maisha ya kiucha mungu.

Kama tunavyoelezwa kwenye mafundisho mbalimbali kuwa dua za mtu aliyetekeleza ibada ya hijja hukubaliwa, ingekuwa busara sana wakaiombea nchi yetu kwa sababu amani ikipatikana ni faida yetu sote.

Kiukweli amani huwa haichagui wala kubagua kijinsia, kabila la mtu, itikadi yake ama vyenginevyo, kwa maana kuwa kila mwana jamii huwa anatumia uhuru kamili wa matumizi ya amani iliyopo.

Pamoja na kwamba Eid ni furaha, lakini wakati huo huo waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla wanapaswa kukumbuka na kuzingatia kwa makini sana kuwa Eid ni ibada.

Kwa maana hiyo maadhimisho na kusherekea kwake lazima kuambatane na msingi ya kiimani na si kufurahiwa kwa mambo maovu na machafu.

Waumini wa dini ya kiislamu waliohalalishiwa sikukuu hii, wanapaswa kutambua kuwa kuisherekea Eid kwa mambo maovu na machafu kama vile zinaa, ulevi, kamari ni kumkosea sana yule aliyeihalalisha sikukuu hiyo.

Aidha ni wajibu wa wazazi na walezi katika jamii kuhakikisha vijana na watoto wanaisherekea vyema sikukuu hiyo kwa kuhakikisha hakuna jambo lolote la madhara linazoweza kujitokeza.

Katika siku kama hizi wapo wenye kuazimia kufanya mambo mabaya ikiwemo wizi na hujuma nyenginezo, ni vyema sana kila mmoja akahakikisha anakuwa mlinzi wa nafsi yake kwanza pamoja na wale waliokaribu naye.

Tunakubali ulinzi wa raia na mali zao ni jukumu la kisheria la jeshi la polisi, lakini mlinzi wa kwanza kabisa wa kuzuia jinai ama kosa lolote ni mtu mwenyewe, na wale waliokaribu yake.

Hata hivyo jeshi la polisi linapaswa kuwa makini katika kipindi hichi na kuwatia mbaroni wale wote wenye dhamira za kutaka kuiharibu sherehe ya Eid.

Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wote wa Shirika la Magazeti ya Serikali, tunawatakia Wazanzibari sikukuu njema ya Eid al Adha.

‘Kul ‘am wa antum bi-khair’