NA ABOUD MAHMOUD
JULAI 18 mwaka huu Zanzibar iliandika historia mpya ya kufanyika mashindano ya kukimbia ambayo yalijulikana kwa jina la Zanzibar International Marathon.
Ni mbio ambazo takriban miaka 20 sasa hazijafanyika na kufanya wananchi wengi kuwa na hamasa ya kushiriki na hata wale ambao hawajashiriki waliweza kutoka nje ya nyumba zao na kutizama washiriki wanavyopita.
Kwa kweli ni jambo la furaha kuona kwamba kwa miaka kadhaa mashindano hayo hayakufanyika na kuweza kurudi tena ambapo wananchi pamoja na serikali wameyaunga mkono.
Lakini pia ni vyema kuwapongeza waliofikiria kuzirejesha tena mbio hizo kwani wamefanya jambo jema na la maana kutokana na kuitangaza nchi kupitia vivutio vilivyopo.
Katika mashindano hayo jumla ya washiriki 3,000 kutoka mataifa mbali mbali kama vile wenyeji Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya,Afrika Kusini, Rwanda, Finland, Ufaransa, Dubai na Uholanzi ambapo ushiriki wao huo naamini utaitangaza vyema nchi yetu.
Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata tunaambiwa kwamba maandalizi ya mashindano haya yalitumia muda wa mwezi mmoja hadi kufanyika kwake.
Hili ni jambo jema na la faraja kwani mwezi mmoja ni muda mfupi kuandaa jambo kubwa kama hilo ukichukulia kuwa jambo hili limefanywa na vijana wadogo tena wazalendo.
Kukamilika kwa jambo hilo kwa muda huo unatokana na bidii yao katika utendaji wao ambao umeweza kusaidia kuitangaza Zanzibar .
Mbali na hilo, lakini kwa upande wa zawadi ya medali waliopata washiriki wa kilomita tano ilipendezesha zaidi kutokana na kuweka aina ya mlango maarufu ‘Zanzibar Door’ ambayo inaelezea alama ya visiwa hivi.
Matumaini yangu kama tutaendelea kuyafanya mashindano haya Zanzibar itaweza kunufaika kwa kukua kiuchumi kupitia sekta mbali mbali.
Lakini hakuna jambo jema lisilokosa changamoto, katika mashindano ya marathoni ya mwaka huu kumejitokeza mambo mbali mbali ambayo kama yatafanyiwa kazi sasa hivi nina amini mwakani yatakwenda vizuri.
Ni lazima waandaji wa mashindano hayo kuwa makini katika kuzitatua changamoto ambazo zilijitokeza mwaka huu na mwakani zisijirudie.
Miongoni mwa changamoto nilizoziona katika mashindano ya mwaka huu ni ile ya madereva wa usafiri wa boda boda kuingia kati katika njia ambazo wakimbiaji wanapita.
Kwa kweli ni jambo baya sana linaloweza kusababisha kuleta atahari kubwa kwa wakimbiaji hao kutokana na madereva hao wa bodaboda wanajulikana uendeshaji wa chombo hicho bila ya kujali wenzao.
Ni vyema kamati ya maandalizi kwa kushirikiana na askari wa usalama wa barabarani kuwa makini na hilo ikiwemo hata kuhakikisha njia hizo zinafungwa na zitumike maalum kwa ajili ya wakimbiaji peke yao.
Lakini mbali na hilo changamoto nyengine niliyoiona ni ile ya askari ambao walikua wamebeba silaha kwa ajili ya ulinzi zilikua zikiwatia khofu wakimbiaji kutoka nje ya nchi kutokana na hali hiyo kuwa hawajaizoea.