TUNIS, TUNISIA

TUNISIA imetumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa, baada ya Rais Kais Saied kuvunja serikali na kuzuia vikao vya bunge.

Hatua hiyo inayoonekana kuungwa mkono na jeshi na kuangaliwa kama ni mapinduzi na wapinzani wake.

Saied amechukua hatua hiyo kufuatia miezi kadhaa ya mivutano kati yake na Waziri Mkuu Hichem Mechichi, pamoja na Bunge lililogawanyika.

Hayo yanajiri wakati ambapo Tunisia inakabiliana na mgogoro wa kiuchumi uliozidishwa na janga la COVID-19.

Saied aliitumia katiba kumfukuza Mechichi, na kuagiza vikao vya bunge visimamishwe kwa siku 30, akisema ameamua kufanya kazi na Wazri Mkuu mpya.

Spika wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi alilaani hatua hiyo na kuwatolea wito raia wa taifa hilo kushiriki maandamano.

Halikadhalika kufuatia hatua hiyo ya Saied, Jeshi la Tunisia limetuma wanajeshi ikulu ya rais mjini Tunis na kuwazuia wafanyakazi wa Serikali kuingia ndani ya jengo hilo.