NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema vyama vya ushirika na kilimo vitapatiwa taaluma ya kilimo bora pamoja na upatikanaji wa pembejeo na masoko kupitia mradi wa KUZA Kilimo Zanzibar.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo maafisa ushirika na wakaguzi kutekeleza mpango wa kuimarisha vyama vya ushirika yanayofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema ofisi yake imefurahishwa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na wakuu wa mradi huo na Idara ya Maendeleo ya Ushirika kwa kuanzisha mashirikiano hayo.

Hivyo, aliwataka wasimamizi wa mradi huo kuendeleza mashirikiano kwa kusaidia utaalamu walionao kwenye vyama vya ushirika kwa lengo la kuviimarisha na kuviboresha pamoja na kuipatia Idara ya Maendeleo na Ushirika ushauri wa kitaalamu.

Aidha aliwaomba wawezeshaji wa mafunzo hayo kuandaa utaratibu mzuri wa kufuatilia matokeo ya mafunzo hayo na kujiridhisha ili kujuwa kama lengo limefikiwa.

Sambamba na hayo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuweka azma ya kuitendea kazi ipasavyo elimu hiyo watakayopatiwa.

“Ni matarajio yangu kwamba kupitia mafunzo haya nitashuhudia mabadiliko makubwa na watakuwa watendaji mahiri na makini na vyama vyao vya ushirika vitatoa tija kwa wanachama wake,” alisema.