NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mkoa wa Mjini Magharibi, imesema maagizo yaliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika majumuisho ya ziara yake itayafanyia kazi kwa vitendo na kwa wakati ili kuona maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waaandishi wa habari, Ofisi kwake akiwa na lengo la kumpongeza Rais, Dk. Mwinyi kwa ziara yake aliyoifanya katika mkoa huo hivi karibuni.

Alisema ni vyema waananchi wakaendelea kutoa ushirikiano na serikali yao na kuahidi kuendelea kusimamia maagizo yote yaliyotolewa ili wannachi wapate huduma za msingi ikiwemo huduma ya maji safi na salama, miundombinu ya barabara na wajasiriamali kupatiwa elimu ya ujasiriamali.

Alisema, kufanyika kwa ziara hiyo katika mkoa wake, Dk. Mwinyi, alionesha dhamira yake ya kuwasaidia wananchi wanyonge kwa kuhakikisha kila Mzanzibari ananufaika na uhuru wa nchi na matunda yalitopo nchini.

“Sote tumekuwa mashuhuda Rais wetu amekwenda kila sehemu inapowagusa wananachi mmoja mmoja na jumla na kuweza kuipitia miradi mbalimbali ikiwemo maji, barabara, na vituo vya afya pamoja na kukutana na wajasiriamali mbalimbali, keroi za ardhi na wavuvi,” alisema.

Alisema serikali ya mkoa haina budi kumpongeza kwani katika uongozi wake amekuwa akishuka kwa wananchi akiwasikiliza changamoto zao moja kwa moja na kuzipatia ufumbuzi kupitia watendaji wake.

Aliongeza kuwa serikali ya mkoa na wilaya zake, watafanya kazi kwa ushirikiano kupitia taasisi za serikali na binafsi zilizomo katika mkoa huo ili kuona malengo na azma ya Dk. Mwinyi kwa wananchi wa Zanzibar yanafikiwa.