NA MWAJUMA JUMA
ZANZIBAR ni miongoni mwa nchi ambayo imejaaliwa na kila aina ya vijana wenye vipaji vya aina mbali mbali ikiwemo vya michezo, sanaa na muziki.
Ukweli ni kwamba unapopita katika visiwa hivi hautachukuwa muda mrefu mara utaweza kukutana na vijana iwe njia au viwanjani wanajishughulisha kwa fani yoyote ile ambayo anaona inampatia manufaa.
Hivyo kutokana na uwepo wa vipaji hivyo Serikali imekuwa nao bega kwa bega katika kuwatafutia wafadhili ambao kwa kiasi kikubwa wataweza kufaidika na vipaji vyao.
Kwa kudhihirisha hilo ni hivi karibuni tu Serikali kupitia wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilitia saini ya mktaba wa miaka mitano na taasisi ya Re-Foccus Africa kwa ajili ya kuendeleza sekta ya michezo, utamaduni na sanaa.
Lengo kuu la mkataba huo ni kuimarisha sekta za michezo na utamaduni hapa Zanzibar.
Aidha mkataba huo umegusa katika mambo mawili kwa ujumla ikiwemo vijana, katika sekta ya michezo, utamaduni na sanaa.
Katika michezo, programu hiyo imejikita zaidi katika kuinua vipaji vya soka, mpira wa Kikapu na kuinua masuala ya riadha kwa kuwapa fursa wanariadha mbali mbali kujifunza mitandaoni na kupata vyeti ambavyo vitatambulika kimataifa ili kuongeza vipaji vyao zaidi.
Hata hivyo kupitia makubaliano hayo taasisi hiyo itatoa mafunzo na kuandaa mashindano ya ndani na ya kimataifa kuhusu riadha.
Yote hayo ambayo yanafanyika yanaenda sambamba katika kutekeleza malengo ya 2050 na kiashirio cha wizara ni kupata medali nyingi za kimataifa kwa kufanya majaribo ya wachezaji wa ndani na kimataifa wa riadha.
Taassisi hiyo itashirikiana na makampuni mengine mbali mbali na klabu zenye umaarufu na vyuo vikuu vinavyojihusisha na mambo ya kimichezo na sanaa ili kuifaidisha Zanzibar.
Ni wazi kwamba vijana ambao watapata fursa hiyo wataweza kufaidika na utaalamu watakaopatiwa huku waalimu wa michezo ambayo imeingizwa kwenye mkataba huo kuongeza ujuzi zaidi.
Kupatikana kwa taasisi hiyo ni njia moja wapo ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kutaka kuendeleza michezo nchini kwa ushirikiano na taasisi binafsi.Pamoja na kwamba sekta ya michezo imetawaliwa na migogoro mbali mbali, lakini, rais baada ya kuapishwa alitoa maelekezo kuhusu sekta mbali mbali ikiwemo ya michezo na moja katika sekta ya michezo.
Katika maelekezo hayo alisema kuwa kuna migogoro na udhamini na kuwataka wadau mbali kusaidia kuendeleza michezo kwa nia moja au nyengine.
Kupitia makubaliano hayo vijana 20 wa Kizanzibari wenye vipaji vya michezo wanatarajiwa kupatiwa udhamini wa kwenda nchini Marekani na taasisi hiyo kupata diploma ya juu ya michezo.
Vijana watakaopatiwa udhamini huo ni wa mpira wa miguu na mpira wa kikapu ambao wenye vipaji na wenye kufanya vizuri katika masomo yao.
Udhamini wa vijana hao utagharimu dola 5000 kwa kila mmoja na watakapokuwepo huko watapata mafunzo ya michezo na ya skuli.Hivyo ni tegemeo letu kwamba Zanzibar vijana wetu watakwenda Marekani kupata mafunzo ya skuli na michezo na hivyo kupata wataalamu wa baadae.
Dira ya 2050 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza uwepo wa idadi ya vijana ambao wamepata mafunzo ya kitaalamu na taasisi hiyo imechangia vijana 20 ambao watakwenda nchini huko.