NA LAYLAT KHALFAN
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, amewataka wazazi kushirikiana na walimu wa madrasa kuwahimiza watoto wao kudurusu masomo yao ili kutimiza ndoto walizojiwekea.
Aliyasema hayo wakati wa mashindano makuu ya kuhifadhi Quran kanda ya Fuoni yaliyofanyika katika skuli ya sekondari ya Aboud Jumbe iliyopo Fuoni, wilaya ya Magharibi ‘B’, Zanzibar.
Alisema malezi yanayozingatia maadili mema, huwajengea mzingira mazuri watoto na kusababisha wawe na maisha bora ya baadae.
Alisema Zanzibar imepata heshima na hadhi kimataifa kupitia watoto wanaoshiriki mashindo ya quran ambao wamelelewa katika malezi yenye ustawi katika jamii iliyowazunguka.
Aidha, Spika alihimiza kudumishwa utamaduni huo hususan kwa watoto wadogo kwani ndio msingi bora wa kuhifadhi Quran.
Alisema ni vyema watoto wakapewa moyo sambamba na nafasi ya kuzingatia zaidi masomo yao ya kisekula na akhera kwa kuwa ndio yana manufaa hapa duniani na ya baadae.
“Endapo watoto watahifadhishwa na kupewa elimu hii mapema itasaidia kuimarisha elimu ya dunia kwa kuwa watakuwa na ufahamu mzuri wa kuzingatia masomo yao,” alisema.
Aidha Zubeir alisema katika kuhakikisha mashandano ya kuhifadhi Quran yanafanikiwa, anadhamiria kuondosha changamoto mbali mbali zinazopunguza ufanisi wake.
Akisoma risala Msaidizi Mshika Fedha wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran kanda ya Fuoni, Hassan Suleiman Khamis, alisema kumekuwa na ugumu kwa baadhi ya watoto kushiriki kikamilifu katika masomo ya dini ikilinganishwa na masomo ya skuli.
“Kupata elimu ya dini ni fursa muhimu sana kwa maendeleo ya watoto lakini siku hizi kumekuwa na changamoto watoto hawadhurii chuoni kwa kisingizio cha kukabiliwa na masomo ya ziada,” alieleza katibu huyo.
Mapema Mwakilishi wa jimbo la Fuoni, Yussuf Hassan Iddi, alisema jukumu la malezi linamgusa kila mmoja kwa nafasi yake, hivyo ni vyema kushirikiana kwa kuhakikisha mafanikio yaliyokusudiwa yanafikiwa.