BRUSSEL, UBELGIJI 

 WANANCHI nchini Ubelgiji wamekaa kimya kwa dakika moja kama ishara ya kuwakumbuka waathirika wa mafuriko yaliosababisha vifo vya watu wapatao 200 magharibi mwa Ulaya.

Watu wasiopungua 31 wamefariki nchini Ubelgiji pekee, huku mamia ya wengine hawajulikani waliko wakati nchini Ujerumani, watu 165 wamefariki huku shughuli ya uokoaji ikiendelea.

Mvua kubwa zilizoandamwa na mafuriko yamesabisha uharibifu mkubwa  katikati miji na vijjii hasa nchini Ubelgiji na Ujerumani ambapo Kansela Angela Merkel amefanya ziara kuwatembelea wahasiriwa wa mafuriko hayo katika mji wa Bad Munstereifel.

Idadi ya watu waliopotea nchini Ubelgiji imepungua katika muda wa siku mbili zilizopita baada ya huduma za mawasiliano kurudi tena na watu zaidi wanafuatiliwa.

Mfalme wa Ubelgiji, Phillipe na Malkia Mathilde wametembelea kituo cha wazima moto cha Verviers, mojawapo ya miji iliyoathirika zaidi na mafuriko.