NA MADINA ISSA

MBUNGE ya Jimbo la Mpendae Taufiq Salum Turky, amesema ubunifu katika shughuli za utalii wa Zanzibar kupitia vyakula utasaidia kuutangaza utalii wa Zanzibar na kupata wageni wengi.

Aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa upishi wa pizza ndefu Tanzania yenye mita 10 iliyopikwa na hoteli ya Park Hyatt kupitia mgahawa wa Beach House uliopo Shangani mjini Unguja.

Alisema kuwa upishi huo umewavutia wageni wengi waliopo katika mgahawa huo ambao umechangia hoteli hiyo kuongeza kipato.

“Ubunifu kama huu ni jambo zuri sana unachangia kuutangaza utalii wa Zanzibar na kama unavyoona leo hapa watu wamejaa kushuhudia uzinduzi wa upishi huu wa pizza ndefu” alisema.

Alisema katika kukuza utalii kutoridhika na watalii kutembelea vivutio vya utalii pekee bali kuwa na ubunifu wa ziada ili kupata faida zaidi.

Hivyo, aliwataka wamiliki wengine wa hoteli kuiga mfano huo na kuwa wabunifu ili kuwavutia watalii kwa sababu watalii wanapenda kuona vitu vipya ambavyo nchini kwao havipo.

Naye Meneja wa hoteli ya Park Hyatt Zanzibar, Nicolas Cedro alisema kuwa lengo la kuandaa upishi huo ni kukuza utalii wa Zanzibar na kuwavutia wageni wanaofika Zanzibar.

Alisema ubunifu huo unakusudia kuisaidia serikali kutangaza vivutio vya zanzibar ili kuimarisha uchumi wake.

Aidha alisema kuwa upishi huo wa Pizza ndefu umewakutanisha watu wa mataifa mbalimbali kujionea na kula chakula hicho ambacho kimenogeshwa na spice za Zanzibar.

Kwa upande wao wageni waliofika katika mgahawa huo, walisema kuwa upishi huo wa piza ndefu yenye ukubwa wa mita 10 ni mara ya kwanza kuwona na umewavutia sana.

Piza hiyo kubwa yenye urefu wa mita 10 ni ya kwanza kutengenezwa nchini Tanzania ambapo waliohudhuria katika hafla hiyo walionesha kuvutiwa na ubunifu huo.