DHANA ya uchumi buluu iliasisiwa na Prof. Gunter Pauli mnamo mwaka 1994 kupitia kitabu chake kiitwacho “The Blue Economy: 10 years – 100 innovations – 100 million jobs”.

Mtaalamu huyo alilinganisha uchumi wa buluu na uchumi wa kijani, kwa kusema shughuli za uchumi wa buluu zina faida zaidi na kuongeza mzunguko wa fedha na matokeo yake ni ya muda mfupi.

Bila shaka mataifa mengi yanayopakana na bahari yanatumia uchumi wa buluu kama njia moja ya kukuza maendeleo ya wananchi wao.

Mafanikio ya utekelezaji wa uchumi wa buluu yanategemea ni vipi nchi husika inatumia na kuhifadhi maeneo yake ya bahari pamoja na rasilimali zake kwa njia endelevu.

Tafiti zinaeleza kuwa sekta zinazohusiana na uchumi wa bahari zinafursa kubwa kuliko sekta nyengine katika ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira.

Kwa upande wa Zanzibar mipango ya maendeleo ya kitaifa ya muda mrefu (Vision 2050), imeweka umuhimu wa kuongeza vipato vya wananchi na kukuza uchumi na kuwa na maendeleo endelevu kupitia uchumi wa buluu.

Hivyo, uwekezaji katika uchumi wa buluu una mazingatio maalum katika kuleta maendeleo ya bahari na rasilimali zake.

Kwa sababu Zanzibar ni nchi ya visiwa, uchumi wa bluu unatarajiwa kuleta faida kubwa kwa kutumia rasilimali za bahari na fukwe kwa njia endelevu ili kukuza uchumi wa nchi, ustawi wa watu, upatikanaji wa ajira na uhifadhi wa mazingira ya bahari.

Bahari ina fursa kubwa na rasilimali zake ni nyingi kama ni chanzo cha nishati, chakula, usafiri wa baharini, kivutio cha utalii ambavyo ni vichocheo vikubwa kwa ustawi wa maisha ya wananchi na ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, rasilimali zinazotokana na bahari zinakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile ongezeko la idadi ya watu, mabadiliko ya tabia nchi, matumizi yasiyoendelevu ya rasilimali hizo, kuwepo kwa maharamia na harakati za maendeleo kama vile ujenzi ambazo kwa kiasi zinatishia usalama wa kutoweka kwa rasilimali za bahari.

Hata hivyo, uchumi unaotokana na rasilimali za bahari, unatarajiwa kutatua changamoto hizo na kuwa ni fursa na nafasi kubwa zaidi kwa ukuaji wa uchumi endelevu wa Zanzibar ambao utaendana na mazingira halisi ya wananchi wa Zanzibar.

Zanzibar kupitia uchumi buluu ina fursa za kuongeza ajira, kukuza usalama wa chakula, kulinda na kusimamia mazingira ya bahari kwa maisha ya sasa na ya baadae.