PARIS, UFARANSA

UFARANSA  imeitaka Tunisia kuteua haraka waziri mkuu mpya na serikali, wakati taifa hilo la kaskazini mwa Afrika likizidi kutumbukia kwenye hali ya kisiasa isiyokua na uhakika.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Yves Le Drian, alimwambia mwenzake wa Tunisia Othman Jerandi kwamba, wananchi wa Tunisia wanasubiri hatua kama hiyo, baada ya rais Kais Saied kufuta kazi maofisa zaidi.

Awali pamoja na kusitisha shughuli za bunge na kuongoza kwa amri ya kiutendaji, hatua ambazo wapinzani wake walisema ni mapinduzi.

Akizungumza kwa njia ya simu na Jerandi, Le Drian alisisitiza umuhimu wa uteuzi wa haraka wa waziri mkuu na kuunda serikali ambayo itakidhi mahitaji ya wananchi wa Tunisia.

Alisema pia kuna umuhimu wa kudumisha utulivu na sheria, na kuruhusu utendaji kazi wa haraka wa taasisi za kidemokrasia za Tunisia.

Mashirika muhimu ya kiraia ya Tunisia yalionya kuhusu kuongeza kinyume cha sheria muda wa siku 30 wa hatua ya rais Saied ya kusitisha shughuli za bunge, na yaliomba katika taarifa ya pamoja, ratiba ya hatua za kisiasa.