PARIS, UFARANSA

RAIS wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza masharti ya kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona, huku ikielezwa kuwa aina mpya ya maambukizi itwayo Delta inaonekana ikisambaa kwa kasi nchini humo.

Macron amesema utoaji wa chanjo utakuwa lazima kwa wahudumu wa afya, huku akitoa wito kwa raia wa nchi hiyo kwenda kupata chanjo, wakati serikali inaanza kuwahamasisha watu kuhusu suala hilo nchini humo.

Mwezi Julai 12 mwaka huu, Emmanuel Macron alitangaza hatua mpya za kuzuia mlipuko wa nne wa aina ya kirusi kipya cha Delta kinachoambukia haraka.

Ikielezwa kuwa hii ni hotuba ya nane ya televisheni ya Rais Macron tangu kuzuka kwa mgogoro huu wa kiafya nchini Ufaransa.

Emmanuel Macron ametangaza chanjo ya lazima kwa wauguzi na wafanyakazi wasio wauguzi katika hospitali mbalimbali, pamoja na kliniki, nyumba za wazee, na pia kwa wataalamu na watu wanaojitolea kwa kuhudumia wazee.

“Wahusika wamepewa muda hadi Septemba 15 kuwa wamefanyiwa chanjo na baada ya tarehe hii, kutafanyika ukaguzi na vikwazo,” alisisitiza.

Aidha Emmanuel Macron alitangaza kuwa kampeni za chanjo dhidi ya Covid-19 zitafanyika kuanzia mwanzoni mwa mwaka wa masomo kwa wanafunzi wa skuli za sekondari na vyuo vikuu.