NA MWANDISHI WETU
IBADA ya Hijja kwa waislamu ni moja ya ibada kongwe na ni miongoni mwa nguzo tano za kiislamu, ibada hii hutekelezwa huko nchini Saudi Arabia kila mwaka.
Kila mwislamu mwenye uwezo hutakiwa kwenda Makka kufanya ibada hii angalau mara moja katika maisha yake ya duniani ambayo ni katika kipindi maalumu kutekeleza ibada ya Hijja.
Waislamu wa Zanzibar na wa dunia kwa ujumla katika kipindi hiki tayari wanakuwa huko Makka nchini Saudi Arabia lakini kwa mwaka jana na mwaka huu ibada hiyo inafanywa na watu kutoka nchi hiyo kutokana na ugonjwa wa corona uliopo sasa duniani.
Ni wazi kuwa wapo wengi ambao walikuwa wameshajipangia kwenda huko Makka kutekeleza ibada hiyo kwa mwaka huu hasa kwa wale waliokosa kwenda mwaka jana lakini kutokana na ugonjwa huo wameshindwa kufanya hivyo, ila Allah (SW) anajua nia yao njema waliyoazimia.
Kama tunavyoelezwa na kitabu chetu kitukufu cha Qur an kuwa Allah Amewaamrisha waja Wake kuitekeleza ibada ya Hijja kwenye Nyumba Tukufu, na kuwalipa malipo mema kutokana na ibada hiyo.
Hivyo yeyote mwenye kuitekeleza Hijja kwenye Nyumba hiyo (Ka’abah) na akawa hakutenda dhambi yoyote, basi atatoka kwenye ibada hiyo hali ya kuwa hana dhambi yoyote mfano wake ni kama mtoto mchanga ambaye ndio kwanza amezaliwa na mama yake. Hijja iliyokubaliwa (Al-Hajj Al-Mabruur) malipo yake si chochote ila ni Pepo.
Aidha wajibu wa Hijja umethibitishwa katika Kitabu cha Allah na Sunnah za Mjumbe wa Allah (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vile vile kwenye makubaliano ya wanavyuoni wa Kiislaam.
Kama mtu yeyote atakaepinga wajibu huu, huyo hana dini, na yeyote anaeacha wajibu huu eti kwa sababu ya kutojali, japo kuwa mtu huyo anaamini, huwa yupo kwenye ukingo wa ukafiri.
Huwaje kwa Muislamu akajihisi kasalimika hali ya kuwa kaipuuza Hijja na ilhali ana uwezo wa kuitekeleza kiafya na kifedha, na anafahamu kuwa Hijja ni wajibu, na ni moja miongoni mwa nguzo za Kiislaamu?
Huwaje kwa Muislaamu kujizuia fedha kuzitumia kwa ajili ya Hijja, na hali ya kuwa anazitumia fedha hizo kwa mambo ya anasa za kidunia?
Huwaje kwa Muislaamu akajihifadhi kutokana na uchovu wa Hijja, lakini anajitahidi kwenye mambo (ya kipuuzi) ya kidunia?
Aidha inakuwaje mtu akawa mvivu katika kuitekeleza Hijja, hali ya kuwa ibada hii imeamrishwa mara moja tu katika uhai wake?
Sambamba na hilo lakini inakuwaje mtu akaakhirisha kuitekeza Hijja, na ilhali hajui kuwa uhai wake utafikia angalau siku moja ijayo au la, lakini kwa hili la zuio la ugonjwa wa corona si miongoni mwa mtu kukataa kutekeleza ibada hiyo.
Hivyo, waislamu ipo haja ya kumuogopa Allah na kutimiza wa wajibu wa Hijja ambao umeamrishwa juu yetu, tuitekeleze kwa dhati ya kumpenda yeye, na kuyakubali maamrisho yake na kuacha makatazo yake.
Ikiwa Muumini ataitekeleza ibada ya Hijja mara moja tu baada ya kufikia baleghe, basi itatosheleza na atakuwa ameutimiza msingi muhimu wa Uislaamu. Hatotakiwa tena kutekeleza Hijja wala Umrah baada ya hapo, isipokuwa ikiwa kama aliweka nadhiri ya kutekeleza moja kati yake, basi atawajibika kuitekeleza nadhiri yake kama tulivyofundishwa na Mtume wetu (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa mfano hivi sasa hapa Zanzibar waislamu wengi hasa wastaafu wamekuwa wakienda kutekeleza ibada ya hijja kutokana na fedha zao za kiinua mgongo, jambo ambalo nia zao zilishaonekana kabla, lakini ugonjwa wa corona imekuwa ni kizingiti kwao.
Kama Serikali ya Saudia Arabia imetoa tamko la kuona ibada hiyo ifanywe na watu wanaoishi nchini humo tena kwa kiwango maalumu, hivyo basi hakuna budi waumini wa dini ya kiislamu kukubaliana na hilo ili kujikinga na ugonjwa wa corona.
Allah atawalipa ujira mwema kwa nia yao thabiti ya kutaka kutekeleza ibada hiyo na ishaallah atawapa mwisho mwema aliowapangia, Ammin.