NA MADINA ISSA

SHIRIKA la ndege Eurowings Discover limelaanzisha safari zake ya kuja Zanzibar kwa ndege ya Airbus A330 – 200 kutoka mji wa Frankfurt Ujerumani, itakayofanya safari zake kwa wiki mara mbili.

Ndege hiyo imefika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), katika kiwanja chake cha Terminal III ikiwa na abiria zaidi ya 60 na kupokelewa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohammed Mussa na viongozi wa Ubalozi wa Ujerumani waliopo Tanzania.

Ndege hiyo ilitua katika uwanja huo majira ya saa 1:20 na kupatiwa heshima ya kumwagiwa maji kama ilivyokuwa na taratibu za kupokea ndege mpta katika viwanja vya ndege.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Lela alisema, ujio wa ndege hiyo itakayokuwa inafanya safari za moja kwa moja kutoka Ulaya hadi Zanzibar, utachangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Zanzibar kama kituo bora cha utalii kwa nchi za bara la Ulaya na ulimweguni kote.

Alisema, serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano na msaada utaohitajika kuhakikisha safari hizo za ndege hiyo ya kampuni ya Lufthansa zinaendelea na kuwa za mafanikio kwa faida ya kampuni hiyo na uchumi wa Zanzibar ambao unategemea zaidi sekta ya utalii.

Sambamba na hayo, Lela alitoa shukurani kwa Shirika la Eurowings DIscover, pamoja na kundi la Lufthansa kwa maamuzi yao ya kuichagua Zanzibar kuwa moja ya vituo vyao vya safari za moja kwa moja kutoka Ulaya.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Mauzo wa Kundi la kampuni za Lufthansa Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dk. Andre Schulz, alisema kampuni za Lufthansa imepanua wigo wake Tanzania, ambapo litatoa huduma za ndege mara sita kwa wiki kuunganisha kati ya miji ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Zanzibar kwa kutumia ndege zake mbili.

Aidha alifahamisha kuwa ndege mpya ya kisasa ya kundi la kampuni za Lufthansa, Eurowings Discover ilitua na kugusa ardhi ya Tanzania kwa mara ya kwanza kabisa ndege hiyo mpya iliruka kuanza safari yake ya kwanza ya abiria kutokea Frankfurt Julai 24.

“Julai 2021 kwa kutumia ndege yake aina ya Airbus A330-200, baada ya kutua

kwa muda Jiji la Mombasa, ndege hiyo namba 4Y134 ilifika uwanja wa Abeid Amani Karume International Airport, asubuhi ya leo saa 1:20 ikiongozwa na rubani Wolfgang Raebiger,” alisema.