JUBA, SUDAN KUSINI

MASHIRIKA ya misaada ya kibinadamu yakiongozwa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, yameendelea kutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi wa ndani waliokimbia makazi yao Equatoria Magharibi huko Sudan Kusini kufuatia mashambulizi ya silaha hivi karibuni.

Taarifa ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS imeeleza kuwa, wanawake, watoto na wazee walikimbia makazi yao kwa kilomita 14 na  hivi sasa wamepiga kambi shuleni na katika kiwanja cha kanisa kwenye eneo laTambura.

Kwamujibu wa taarifa kutoka kwa wakimbizi hao wanasema kwamba hawakuwa na hiari zaidi ya kuacha kila kitu chao na kukimbia wakati magenge yenye silaha yalipovamia kwenye vijiji vyao, yakichoma vibanda vyao na kufyatua risasi hewani.

“Tuna watu kadhaa ambao bado hawajulikani waliko na hii inasikitisha sana. Wengine wanatafuta waume zao, baba zao, na watoto wao ambao wamepotea” alisema ofisa wa Umoja wa Mataifa

Aidha hivi karibun Wanasiasa wawili wenye nguvu zaidi Sudan Kusini, Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar, walitoa hakikisho kuwa hawataongoza nchi hiyo kurudi vitani wakati wanaadhimisha miaka 10 ya kujitenga na Sudan na kupata Uhuru.

Vurugu ziliibuka nchini Sudan Kusini mwishoni mwa mwaka 2013, miaka miwili baada ya kujitenga na Sudan, wakati Rais Salva Kiir, wa kabila la Dinka, alipomfuta makamu wa rais Riek Machar, kutoka kwa kundi pinzani la Nuer ambaye alituhumiwa kuwa alipanga kuipindua serikali.

Wawili hao sasa wamesaini mikataba kadhaa kumaliza vita ambayo, inayochochewa na mivutano ya kikabila iliyodumu kwa muda mrefu, na ambayo inakadiriwa kuua zaidi ya watu 400,000, ikiwa mwaka huu Kiir na Machar waliafikiana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.