NA ASHA MAULID ALI (Wakfu)

  • Humfanya mja kuwa karibu na Mola wake

  • Humtengenezea mja maisha bora ya Akhera

LABAYKA Allaahumma Labbaik, Labbayka laashariika laka labbaik, Innalhamda waneemata lakawalmulk, laashariikala”. Huu ni wito wa yule Muumini wa kiislamu aneitika kwa Mola wake, ambae ameweza kumuwelekea Allah (SW) kwa kutekeleza nguzo ya tano ya Kiislamu ambayo inamlazimu kila Muislamu mwenye uwezo wa kisiha na kifedha kwenda kutekeleza ibada hiyo nayo ni ibada ya Hijja.

Mwandishi wa makala hii amekusudia kukujuza juu ya mustakabali mzuri wa ibada ya Hija kwa Waislamu ambayo inalazimika kuitekeleza mara moja tu katika umri wa mwanaadamu, kwa kuzingatia masharti na vigezo vilivyowekwa na shariah ya kutekeleza ibada hii.

Hijja ni kuizuru Kaaba (Nyumba takatifu ya Allah (SW) katika mwezi na siku maalum. Utekelezaji wake na matendo yote yanayokamilisha ibada ya hijja yamewekwa wazi katika Qur-an na Sunna.

Hata hivyo, ibada ya Hijja haikuanza kufaradhishwa katika Umma wa Mtume Muhammad S.A.W) bali ibada hii imefaradhishwa kuanzia zama za Nabii Ibrahim (A.S) kama tunavyosimuliwa katika Qur-an aya 27 SuratulAlhajinayosema.

“Na watangazie watu Hijja, watakuja kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyeyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali” Kwa lengo la utiifu wa kweli pamoja na kuwajengea ukaribu baina ya Mola na Waislamu.

Mbali na kuwa ibada ya hijja ina malipo makubwa kutoka kwa Allah (SW), lakini kwa upande mwengine, hijja ni muhimu sana. Ina faida nyingi katika mwenendo mzima wa maisha ya mwanaadamu hasa waislamu na hii ni miongoni mwa neema kubwa za Mwenyezi Mungu(SW) kwa Waja wake.

Miongoni mwa faida na umuhimu wa ibada ya hijja ni kupata msamaha na kufutiwa madhambi yote ya aliehiji.  Mtume (S.A.W) Amesema “Mwenye kuhiji na akawa hakufanya uchafu wowote wala kuzungumza maneno machafu basi hurejea kama siku aliyozaliwa na Mama yake (hana dhambi).

Vile vile Mwenyezi Mungu husamehe dhambi za wanaosimama Arafaat. Dalili ya hili, ni pale Mtume (SAW) aliposimama Arafaat na akamuamrisha Bilal (R.A) awatulize watu waliokuwepo katika uwanja ili awambie kuwa ameteremshiwa wahyi na Jibril kuwa Allah SW amewasamehe watu wote waliokuwepo kwenye viwanja vya Arafaat.

Hata hivyo Sayyidna Omar akauliza Jee? Ni kwa ajili ya sisi tu tuliokuwepo hapa? Mtume akajibu ni kwa ajili yetu na watakaokuja kwenye uwanja huu wa Arafa hadi Kiama. Kwa mfano huu, ni wazi kuwa tunapofanya ibada hii tunanufaika kwa kufutiwa madhambi.

Nafasi ya mja kuwa na utulivu

Faida nyengine ambayo mja huipata pindi anapofanya ibada ya hija ni kuiweka nafsi yake na kuiandaa na safari ya akhera, ambayo kila mmoja wetu itamkabili.

Aidha ibada ya hijja ndio kimbilio la waja huko huonyesha unyenyekevu wao mbele ya yule aliyewaumba hufanya, mengi mazuri hutaraji kutoka kwake ikiwemo kutakaswa nafsi zao na machafu, kutengeneza tabia zao na kuwa karibu na Mola wao.

Kujenga umoja.

Umoja ni katika misingi ya dini ya kiislamu. Jambo la kwanza alilolifanya Mtume (S.A.W) alipofika Madina kwa wafuasi wake ni kuwaunganisha na ndio dini ikapata nguvu. Hijja inajenga umoja kwa kuwakutanisha waislamu wote duniani katika maeneo hayo matukufu bila ya kujali nafasi ya mtu, cheo, elimu, kipato, ubora wa makabila nakadhalika.

Wote hujumuika kwa lengo la kumtukuza Mola wao wakiwa katika vazi moja, matendo ya ibada yote huyafanya kwa pamoja. Umoja huu haupatikani isipokuwa katika ibada ya Hijja nani fakhari kwa waislamu.

Kujikurubisha kwa Allah (SW).

Faida nyengine ya ibada ya Hijjani Mja huwa karibu na Mola wake kwa kupata faragha ya kufanya ibada zenye ujira mkubwa katika maeneo hayo matakatifu anayoyapenda Mwenyezimungu.

Mwenye kuhijji hujitoleakwa mali, nafsi na muda wake pale, anapoiwacha familia yake na kwenda kutekeleza ibada kwa ajili ya Mola wake.

Kutengeneza maisha bora ya Akhera.

Waumini wa kiislamu wanaamini kuwa baada ya maisha ya Duniani kuna maisha mengine baada ya kifo ambayo ni Barzakh. Hapo husubiria maisha ya Akhera ambayo ndio maisha hasa anayotakiwa ayaande huku duniani ili akapate maisha bora.

Bila shaka, yule aliyefuata maamrisho ya Mwenyezi mungu, ikiwa pamoja na kutekeleza nguzo za Uislamu na kuwa mfuwasi bora wa Mtume Muhammad (SAW), atalipwa malipo makubwa na kupata maisha mazuri.

Inaonyesha wazi kuwa Ibada ya hijja ina umuhimu na faida kubwa kwa Waislamu, Kwa kutambua umuhimu huo sharia ya kiislamu ikajuzisha kuhijiwa kwa wale wenye dharura au wale ambao wametangulia mbele ya haki kabla ya kufanya ibada hiyo takatifu.

Kwa mujibu wa Sharia inamlazimu yule atakae muhijia mtu na yeye awe ameshakwenda kuhiji.

Mwandishi wa Makala hii amezungumza na mmoja kati ya wanadhimu wanaojishughulisha na kusafirisha mahujaji na kueleza kuwa.

“Sharia ya kiislamu ni nyepesi kwani imezingatia hali zote za watu na kuhakikisha kila mtu anakuwa na fursa sawa na mwengine katika kuitengeneza akhera yake kwa mfano mtu ambae amefariki au mgonjwa ambae hawezi kufika katika maeneo ya ibada mtu huyo anaweza kuhijiwa na hupata ujira kama kwamba amehiji yeye mwenyewe.

WENYE KIPATO KUSHINDWA KUTEKELEZA IBADA YA HIJJA

Mbali na waislamu kujua umuhimu wa ibada ya Hijja, lakini wapo ambao wamejaaliwa kipato kikubwa kinachowawezesha kutekeleza nguzo ya Hijja ambayo ni wajibu kwa kila mwenye uwezo, lakini bado mpaka hii leo hawajaitikia wito huo wa kutekeleza wajibu huo pasi na sababu yoyote.

Hawa wanajijengea maisha mabaya ya baadae na kujiondolea baraka kwa vile wanavyovichuma, Na hapa lazima tufahamu suala la mtu kuwa na uwezo kisheria likoje?

Kwa mfano mtu anamiliki nyumba 2 mpaka 3 na mashamba mawili ambayo yamesheheni miti na nafaka tofauti na vinavyomuingizia kipato cha kutosha.

Au wenye kumiliki maduka ya bidhaa mbali mbali za biashara, lakini wanajihesabu kuwa hawana uwezo kwa kudhania tu ili mtu awe na uwezo awe ana fedha taslimu ambazo zipo benki au zimekaa bila ya kufanyia chochote hapo ndo mtu anajihesabu hana uwezo.

Huu ni ufahamu mbaya na unakwenda kinyume na sheria, Makusudio ya uwezo ni kumiliki kile ambacho kitakufikisha katika maeneo ya Ibada na kuwa na akiba ya kuiwachia familia kwa mahitaji yao kwa kipindi chote ambacho utakuwa safarini mpaka kurudi kwako.

Hatusemi mtu auze nyumba halafu abaki hana pa kujistiri yeye na familia yake, lakini mwenye kumiliki nyumba tatu au nne huyu ibada ya hijja inamuwajibikia na anahesabiwa ni mwenye uwezo na akifariki leo basi atafariki akiwa na dhima ya iabada hiyo.

Kwa maelezo hayo inatupasa tujifunze kupitia kigezo chetu na Mtume wetu Muhammad (SAW) na masahaba wake.

Haikuwazuia kutekeleza ibada ya Hijja kwa kusubiri wamiliki mamilioni ya fedha au nyumba 10 na mashamba, bali walitekeleza ibada hiyo kwa kile ambacho walikimiliki kuwawezesha kufika katika Kaabah.

Na Mtume (S.A.W) kawakemea vikali wale wenye uwezo na wasihiji mpaka yanawakuta umauti kwa kusema “Mtu ambae atamiliki masurufu ya safari na kipando cha kumfikisha katika nyumba ya Mwenyezi Mungu (Kaabah) na asihiji, basi haikuwa kifo cha mtu huyo ila ni kifo cha Myahudi au Mnasara(Mkiristo)” hii ina maana kwamba atakaekufa hali ya kuwa hajahiji na uwezo anao atakufa kifo cha kikafiri.

YANAYOMUWAJIBIKIA HAJJI, HAJJAT KABLA YA IBADA YA HIJJA

Maandalizi kwa yule alieazimia kwenda kutekeleza ibada ya Hijja zipo aina mbili (2) maandalizi, ya kiroho na kiwiliwili.

MATAYARISHO YA KIROHO

Kwa upande wa matayarisho ya kiroho, muislamu mwenye kuazimia kufanyaibada ya Hijja anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

 

KUOMBA MSAMAHA KWA MWENYEZINGU

Istighfar ni jambo la lazima kwa kila mtu na kila siku unatikiwa umuombe msamaha mola wako kwa makosa uliyoyafanya. Mtume Muhammad (SAW) pamoja na kwamba alisamehewa dhambi zake zote zilizopita na zijazo lakini alikuwa akiomba msamaha kwa siku mara 70 na sisi je?

Ni wajibu wetu kuomba msamaha, haswa kwa yule anaetarajia kwenda kufanya ibada ya Hijja. Anatakiwa alipe kipaumbele suala la kuomba msamaha kwa sababu ni ibada inayohitaji ufaragha wa nafsi na moyo.

Alhaaji au Hajjat mtarajiwa anapofunga safari akiwa bado hakusafishiana nia na wale aliokwazana nao basi utulivu wa ibada hiyo hautokuwepo. Aidha athari kubwa zaidi anayoipata huenda ikawa hata yale maombi yake atakayoyafanya na dua zake zisikubaliwe.

Imepokewa kuwa Mtume SAW amesema “Watu wa aina tatu hawakubaliwi maombi yao wala ibada zao miongoni ni mwenye kukata ujamaa na ndugu wawili wenye ugomvi baina yao” sasa vipi mja ataridhia kumkabili Mola wake hakuwa akitambua kuwa anachokitarajia hatokipata?

Hii ina maana kuwa lazima kwa mwenye kuazimia kufanya ibada ya Hijja, kwanza ajisafishe nafsi yake kwa kumuomba msamaha Mola wake, wazee wake, walezi, Mashehke zake, walimu wake ndugu na jirani zake waliomzunguka na kila anaetakikana kumfanyia wemaili, akafanye ibada iliyokamilika na kupata ujira ule ambao Mwenyezimungu amewaahidi kuwalipa waliohija hija zilizokamilika .

KUZITAKASA IBADA ZAKE NA KUZIFANYA KWA AJILI YA ALLAH (SW).

Lengo kubwa la kuumbwa mja kumuabudu muumba, Ibada ili ikubaliwe basi ifanywe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu Wengi Wetu tunaziharibu ibada zetu na kutokukubaliwa kwa sababu ya kuzichanganya na kitu kinachoitwa Riyaa (kujionyesha).

Unapofanya ibada ikawa lengo lako ni kusifiwa na watu, au kuitwa Alhaj au kwa malengo yako ya kidunia, hiyo ni kwamba ibada ulioifanya sio kwa ajili ya Mola wako.

Ibada kama Hijja ni ibada yenye gharama za mali, wakati nakadhalika. Inampasa mja aifanye kwa ajili ya Mola wake ili apate malipo makubwa na kukubaliwa kwa ibada zake, kinyume na hivyo atakuwa amepoteza muda na mali na atarudi bila kufaidika na ibada zake.

KUREJESHA HAKI KWA WALE ALIOWADHULUMU

Madeni na haki za watu ni suala zito sana, pamoja na kwamba watu wengi huliona jepesi. Mtume SAW amesema “Husamehewa shahidi (aliyekufa vitani kwa ajili ya kunyanyua neno la Mwenyezimungu) kila dhambi aliyoifanya isipokuwa deni”.

Kwa kupitia maneno haya ndio utaona uzito wa deni, haki za waja, na uzito wa dhulma. Hayo yote Mwenyezi Mungu hayamfurahishi na anachukia zaidi dhulma na ndio maana hata yeye mwenyewe pamoja ukwasi wake na utukufu alionao amejiharamishia kudhulumu au kumkosesha mtu mja wake haki yake.

Amesema katika Qur-an “Na hakuwa Mola wako ni mwenye kuwadhulumu waja wake”. Akasema Mtume SAW katika hadithil Qudusy: “Enyi waja wangu mimi nimejiharamishia dhulma kwa nafsi yangu basi msidhulumiane”.

Dhulma sio kitu kizuri na kumzuilia mtu haki zake ni haramu. Malipo ya anaedhulumiwa siku ya kiama ni kuchukuliwa thawabu zake na kulipwa aliemdhulumu, na asiekuwa na thawabu atambebea mizigo yake ya dhambi hivyo, kumpelekea kuingia katika moto wa Jahannam na ndio mana ikasisitizwa kwa wale wanaotaka kwenda kuhiji kurejesha haki za watu ili kujisafisha.

MAHUJAJI WANATAKIWA KUFANYA MAMBO HAYA ILI HIJJA ZAO ZIWE MAKBUUL

KUJIPAMBA NA SIFA YA UCHAMUNGU

Uchamungu ni sifa ya muumini wa kweli na hakuna chochote anachokiangalia Mwenyezimungu kwa mja zaidi ya uchamungu neno hili ndio lililokusanya kila kitu ambacho mja anatakiwa akifanye iwe katika matendo mema au kujiepusha na makatazo.

Uchamungu ndio pambo la Muislamu na ndio ngao yake ili aweze kuvuka vizingiti vya dunia na kupata maisha bora huko akhera, Hivyo kwa anaetaka kwenda kufanya ibada takatifu ya Hija ni lazima ajipambe na sifa ya uchamungu na kujiweka karibu sana na Mola wake.

Inampasa Alhaj kujiepusha na mambo machafu yasiompendezesha Allah, kama kusema maneno machafu, kubishana na mijadala inayoondoa muruwa na kuvunjiana heshima.

MAANDALIZI YA KIWILIWILI NA MALI

 

Maandalizi haya atayafanya kwa kuzingatia yafuatayo:-

kuandika wasia, kurejesha amana za watu (Deni), Kufanya vipimo vya afya na matibabu, kuhijji kwa chumo au mali ya halali, kufanya mazoezi na kuwachia familia mahitaji yao yakujikimu.

 

KUANDIKA WASIA

Wasia ni kujitolea haki ambayo utaiegemeza kwa mtu mwengine baada ya mtu kuondoka duniani, Katika wasia unaweza kumuusia mtu juu ya mustakbali mzima wa mali au majukumu yako, ni vyema kwa anaetarajia kwenda kutekeleza ibda ya hijja aweke wasia kabla ya kuondoka kwa vile safari inachukuwa siku nyingi na faida kubwa ya wasia hupunguza migogoro mtu inapotokea amefariki.

Hata hivyo wasia haundikiwi kwa warithi au zaidi ya thuluthi ya mali.

KUREJESHA AMANA ZA WATU

Amana ni kitu ambacho kimekosekana katika jamii yetu ya leo. Watu wamekosa uaminifu na ndio maana Mwenyezimungu akajaalia kuondoka kwa amana ni moja kati ya dalili za kiyama.

Mtu unapoaminiwa inapasa ujiaminishe, hivyo basi ikitokea umeweka azma ya kufanya hijja na una amana za watu ni juu yako kuzirejesha ili kuepusha mchanganyiko wa mali zako na mali za watu wengine pindi utakapokufa Au haki za watu zikapotea kwa kutokujuulikana wenyewe. Aidha unajipunguzia wewe mwenyewe mizogo mbele ya Mola wako kwa sababu haki zote hizo zitabaki kama ni madeni yatakayofungamanishwa nawe.

MAHITAJI YA FAMILIA

 

Kuwaachia mahitaji ya kutoshawanaokulazimu tokea unaposafiri mpaka utakaporudi. Hata Kama mke anakazi yake, ni wajibu kwa mume au baba wa familia kuwachumia wanaomlazimu wawe ni watoto, wazee au mke Jukumu hilo halitoanguka kwa sababu ya kwenda kutekeleza ibada ya Hijja.

 

Kinyume chahivyo utatoka katika kundi la wale wenye uwezo, Si vyema wala haifai kuiwacha familia ikiomba na kuhangaika huku na kule kwa kuwa tu unalazimisha kwenda kufanya ibada ya Hijja.

 

Jukumu la kutunza familia ni kubwa zaidi na linahitajika kutiliwa mkazo kwa kuhakikisha unamtimizia mahitaji ya umuhimu kuliko kufanya ibada ya Hijja ikiwa huna wasaa huo basi itumikie familia mpaka utakapopata uwezo wa kufanya hijja.

 

KUPIMA AFYA

 

Na vizuri kwa anaetaka kwenda hijja kwa kufanya vipimo vya afya hiyo itasaidia kugunduamapema magonjwa yanayomsumbua. Ibada ya hijja inahitaji watu wenye afya na wasiokuwa na magonjwa hasa yenye kuambukiza.

Mjumuiko mkubwa ambao unaokuwepo huko. Si vyemakwa wenye maradhi yenye kuambukiza kuficha kwa hiyo inaweza kusababisha madhara kwa waliowengi na utakuwa umesababisha matatizo kwa wengine bali unaweza ukasababisha vifo.

 

Tunawanasihi wote tunakwenda kuhiji tukiwa wazima wa afya ili tuweze kufanya ibada zetu kwa utulivu zaidi.  Hii pia itakusaidia kupata ushauri wa madaktari hata kutibiwa kwa yale maradhi ambayo ya naweza kutibika.

KWENDA HIJJA KWA CHUMO LA HALALI.

Kwa vile hijja ni wajibu wa kila muislamu aliyekuwa na uwezo, hivyo hapana shaka anaetaka kuhiji akahakikisha safari yake yote anafanya kwa kutumia pesa zahalali. Mwenyezimungu ni mzuri na anapenda vilivyovizuri.

Chumo la halali linajumuisha kivazi unachovaa, kipando utakachopanda kwa wanotumia vipando vyao binafsi, fedha utakayotumia kwa ajili ya mahitaji mbali mbali vyote viwe vya halali. Kuhiji kwa mali ya haramu au yenye shubha inapelekea kutokukubalika kwa amali hiyo tukufu.

Ibada ya Hijja ni wajibu wa kiimani na lina faida nyingi, Hata hivyo pamoja na kuuwa ni wajibu kwa wenye uwezo, watu wengi wanatamani wahiji pamoja na kuwa uwezo wao kiuchumi ni mdogo.

Wapo wanaotumia mafao yao ya kustaafu nakadhalika, Serikali ya Mapinduziya Zanzibar kwa lengo lile lile la kuwasaidia na kuwahudumia Wananchii wake imeamuakuanzisha Mfuko wa Hijja kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.

Uzoefu wa Nchi nyingi unaonesha kuwa Mfuko ya Hijja huwasaidia Waislamu wengi wamudu kuitekeleza ibada hiyo kwa kuchangia kidogo kidogo.

Ili kufafamu zaidi kuhusu Mfuko huo wa Hijja fuatilia Makala zijazo.

 

 

Waumini wa Zanzibar wakiwa katika uwanja wa ndege wakati wakirudi kufanya ibada ya Hijja