Jamii inapaswa kufuata maelekezo ya Serikali, wataalamu wa afya

NA HUSNA MOHAMMED

KATIKA wimbi hili la tatu la ugonjwa wa corona, nchi kadhaa duniani zimekuwa zikitoa muongozo namna ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo kwa raia wake.

Kwa mfano hapa Zanzibar hivi sasa zoezi la chanjo linaendelea kwa baadhi ya watu maalumu wanaotoa huduma za watu wengi kwa wakati mmoja tayari wameanza kupokea chanjo hizo.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kuwa uvaaji wa barakoa bado ni muhimu kwa sasa huku Serikali ikisubiri kuwapa chanjo wananchi wake kwa hiari.

Katika makala haya yaleo tutazungumzia namna ya uvaaji wa barakoa ili kujikinga na ugonjwa wa corona.

Barakoa ni kitambaa kinachovaliwa usoni au kichwani na kwamba hutegemea aina ya barakoa yenyewe, ziko zile zenye tundu kwenye macho, pua na mdomo nakadhalika.

Barakoa za kinga hutumiwa kulinda uso au sehemu zake (mdomo, pua, nakadhalika) na viungo vya kupumua dhidi ya kuzuiya maambukizi ya maradhi au athari yeyote kwenye uso.

Katika Makala haya tutazungumzia aina za barakoa na uvaaji wake hasa katika wakati huu wa kujikinga na gonjwa hatari la maambukizi ya Corona.

AINA ZA BARAKOA (MASK)

Ziko aina mbalimbali za barakoa zinazovaliwa kwa shughuli mbalimbali kama hivi zifuatazo ikiwa ni pamoja na zile zinazozuia au kupunguza athari na hatari za vumbi, gesi, hewa chafu au viini vya ugonjwa.

Katika mazingira ya hospitali kuna aina mbali mbali za barakoa zinatoa ulinzi wa viwango tofauti kama vile barakoa inayotoa ulinzi bora zaidi ni FFP3 au N95 au FFP2 ina kifaa cha kupumilia ambacho kina uwezo wa kuchuja hewa mtu anayovuta.

Barakoa hizi za kinga dhidi ya maambukizi, zinazovaliwa na watu wakihudumia wagonjwa au wakihofia maambukizi wakati wa mlipuko wa ugonjwa kama vile ebola, kipindupindu, covid 19 nakadhalika ambazo zinajulikana kwa jina la N95 barakoa

Wataalam hawashauri umma kutumia hizi kwa kuwa ni makhsusi kwa ajili ya wahudumu wa afya ambao wapo karibu zaidi na wagonjwa wa corona na wale wa magonjwa ya kuambukiza ambao hujilinda katika hatari kubwa ya kukumbana na majimaji ya njia ya hewa kutoka kwa waathirika.

Barakoa za kimatibabu (surgical mask), zinazovaliwa na daktari wakati wa upasuaji, mbali na hivo barakoa hizi ni gharama maana inashauriwa kuvaliwa kila baada ya masaa  mawili mpaka manne katika sehemu maalumu (kwenye vyumba vya upasuaji) kwani  kwenye chumba cha upasuaji kinaweza kuhimili  masaa hayo kutokana kuwepo wa kiyoyozi.

Kwa kuwa virusi vya corona vinaweza kusambazwa kwa matone ambayo yanaweza kusambaa hewani, pale ambapo wale walioambukizwa wakiongea, wakikohoa au kupiga chafya.

Virusi hivyo vinaweza kuingia mwilini kupitia macho na mdomo au au baada ya kugusa vitu vilivyopata maambukizi.

Barakoa za vitambaa (Cloth mask) ambazo sasa hivi zinatumiwa na jamii  katika dunia hii ilioingiliwa na janga hili la corona duniani kote.

Barakoa ya kitambaa kizito kama kitenge ni vizuri kuviunganisha viwili pamoja na vipeto yaani mikunjo na vitambaa laini inatakiwa alau iwe na leya mbili na ile ya kitambaa chepesi mpaka leya tatu ikiambatana mikunjo yake, hizi unaweza kuzivaa angalau masaa manne lakini zinatakiwa zivaliwe kwa utaratibu maalumu kutokana muongozo wa wizara ya afya.

FAIDA YA UVAAJI WA BARAKOA

Faida kubwa ni kujikinga na magonjwa ya kuambukiza kama haya ya janga la corona kwa sasa

Kwa mfano hizi barakoa za vitambaa kama za vitenge na nyenginezo mvaaji anaweza kuzivaa zaidi ya mara moja ikiwa utaziweka katika hali ya usafi, gharama yake ni ndogo sana kama shilingi 1,000 mpaka 1,500.

Sambamba na hilo, lakini pia barakoa hizi husaidia kutochafua mazingira kama zilivyo zile za wahudumu wa afya ‘surgical mask’.

Kwa maana hiyo basi jamii inashauriwa kuvaa mask za vitambaa kwa kufuata ushauri na muongozo uliotolewa  na Wizara ya Afya itakayosaidia kujikinga na maradhi ya maambukizi kama haya ya covid 19 pamoja na maradhi mengine yanayoweza kuambukizwa kwa njia ya hewa.

NAMNA YA UVAAJI WA BARAKOA

Kuhakikisha anaetaka kuvaa barakoa ananawa mikono kwa maji ya kutiririka na sabuni au vitakasa mikono kabla ya kuvaa barakoa.

Aidha ahakikishe barakoa yake haina tunduau uwazi wowote sambamba na upande wenye chuma laini unakaa juu na upande wa ndani unakuwa mweupe.

Pia mvaaji wa barakoa anatakiwa kuhakikisha barakoa yake inabana vizuri usawa wa pua, kuivuta barakoa usawa wa chini ya kidevu.

Sambamba na hilo lakini mvaaji wa barakoa hatakiwi kuigusa sehemu ya nje ili kuepuka maambukizi mapya ya virusi na endapo kwa bahati mbaya ikatokezea kuigusa ahakikishe ananawa mikono kwa sabuni au vitakasa mikono.

NAMNA YA KUFANYA KWA BARAKOA ILIYOTUMIKA KWA MVAAJI

Anatakiwa mvaaji kuweka barakoa yake kwa kushika Kamba au mpira ulioko nyuma ya sikio na kuivutia mbele bila ya kushika sehemu ya mbele ya barakoa.

Ni lazima kuhakikisha wakati wa kuvua barakoa huigusi sehemu ya uso sambamba na kuitupa kwenye chimbo maalumu cha kuhifadhia taka na si kutupa ovyo kama ilivyo sasa kwa baadhi ya maeneo majiani.

Pia kuhakikisha kuwa mtu ananawa mikono kwa maji ya kutiririka mara baada ya kuitupua barakoa.

Hivyo, jamii haipaswi kuwa wakaidi hasa katika kipindi hiki cha kupambana na ugonjwa wa corona kwa kuwa wako baadhi ya watu wamekuwa wakikaidi agizo la serikali jambo ambalo linaweza kusababisha matatizo makubwa katika kupamabana na ugonjwa huu.

Ni wazi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, imekuwa ikiwajali watu wake hasa kutokana na hali ngumu ya uchumi, hivyo haipaswi kabisa jamii kupuuza maelekezo ya wataalamu wa afya katika kujikinga na magonjwa ya kuambukiza kwa njia ya hewa ikiwemo barakoa.

Kwa mfano shughuli za mikusanyiko ya watu kama vile masokoni, kwenye magari na maeneo mengine ya mikusanyiko ni muhimu sana kuvaa barakoa ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo corona.

Ugonjwa huu wa corona tutaweza kuushinda ikiwa kila mmoja atatekeleza maagizo ya serikali nay a wataalamu wa afya.