JUBA, SUDAN KUSINI

TUME ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) imesema inapanga kuanzisha mpango mpya muhimu ambao utaongeza ushiriki kwenye mchakato wa amani na juhudi za kuunga mkono ili kuendeleza mkakati wa Kufufuliwa Makubaliano.

UNMISS imesema mpango wake wa amani utawaleta pamoja washiriki kutoka majimbo kumi na maeneo matatu ya kiutawala katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji, ukianzia na shughuli mfululizo za utoaji elimu na kukuza uelewa mjini Juba.

Inaelezwa kuwa mpango huo unategemewa kuzinduliwa baadaye wiki ijayo, ambapo itafanyika hafla maalumu inayoongozwa na mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa UM Nicholas Haysom na Makamu wa Rais Rebecca Nyandeng De Mabior, wakisaidiwa na wawakilishi wa IGAD na AU.

Hivi karibun Wanasiasa wawili wenye nguvu zaidi Sudan Kusini, Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar, walitoa hakikisho Ijumaa kuwa hawataongoza nchi hiyo kurudi vitani wakati wanaadhimisha miaka 10 ya kujitenga na Sudan na kupata Uhuru.

Vurugu ziliibuka nchini Sudan Kusini mwishoni mwa mwaka 2013, miaka miwili baada ya kujitenga na Sudan, wakati Rais Salva Kiir, wa kabila la Dinka, alipomfuta makamu wa rais Riek Machar, kutoka kwa kundi pinzani la Nuer ambaye alituhumiwa kuwa alipanga kuipindua serikali.

Wawili hao sasa wamesaini mikataba kadhaa kumaliza vita ambayo, inachochewa na mivutano ya kikabila iliyodumu kwa muda mrefu, na ambayo inakadiriwa kuua zaidi ya watu 400,000. Mwaka huu Kiir na Machar waliafikiana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.