LONDON, UINGEREZA

NAIBU Mkuu anaeshughulikia masuala ya kibinaadamu katika Umoja wa Mataifa, Ramesh Rajasingham amesema janga la Covid-19 limeyaathiri zaidi kwa mwaka huu mataifa yenye mizozo na masikini ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Akizungumza katika mkutano wa ndani wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ofisa huyo mwandamizi alisema hali hiyo ilichochewa zaidi na ukata wa upatikanaji chanjo, matatizo ya huduma za afya pamoja na kusambaa kwa aina mpya ya kirusi cha corona kiitwacho Delta katika mataifa 124, yakiwemo tete 17 na yenye mizozo.

Katika taarifa yake hiyo Rajasingham alisema kwa mwaka 2021, karibu robo tatu ya mataifa yanahitaji misaada na kumekuwa na rikodi za visa vingi vya maambukizi au vifo kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita.