JUBA, SUDAN KUSINI

MFUKO wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia Watoto (UNICEF), wamesema kuwa watoto zaidi ya milioni nne wanahitaji msaada wa dharura kutokana na mzozo wa muda mrefu nchini Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo, taifa hilo ambalo linaadhimisha miaka 10 baada ya kupata uhuru, Julai 9, 2011, linaendelea kukabiliwa na mizozo mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Aidha, shirika hilo la lilionya kuwa maisha ya watoto nchini humo ni taabu sana kwa sababu maisha yao yanaathiriwa na machafuko.

Umoja huo umeongeza kusema kuwa maisha ya watoto wengi nchini humo ni ya dhiki hasa ikizingatiwa kuwa wanakumbwa na ghasia, utapia mlo na changamoto mbalimbali.

Rais Salva Kiir na Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar wameungana kutekeleza makubaliano ya mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018, hata hivyo changamoto za watoto bado hazijatatuliwa nchini humo.

Ripoti sawa na hiyo ya UNICEF pia imetolewa kwa taifa jirani na Sudan Kusini la Sudan, ambapo shirika limeonya kwamba watoto milioni tatu wenye umri wa chini ya miaka tano wanasumbuliwa na utapiamlo.

Saji Abdullah, Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, alisema kuwa karibu watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka mitano nchini humo wana utapiamlo, na kuongeza kuwa 570,000 kati yao wako katika hali mbaya.