BUJUMBURA, BURUNDI

KIONGOZI wa chama kikuu cha upinzani nchini Burundi, Agathon Rwasa, amesema anaguswa na mtukio ya kutekwa nyara kwa viongozi wa chama chake, huku akilitolea mfano tukio la Ijumaa ya wiki iliyopita ambapo kiongozi wa chama hicho Elie Ngomirakiza alitekwa nyara kwenye kitongoji cha Mutimbuzi jijini Bujumbura.

Kwa mujibu wa Rwasa, Elie alitekwa nyara na watu wasiofahamika ambao walikuwa katika gari ya kijeshi.

Huku taarifa ya chama hicho ikisema, Elie alitekwa wakati alipokuwa akitoka kwenye eneo lake la kazi kupeleka matofali ya kujengea kwa mmoja ya wateja wake mjini Bujumbura.

Aidha kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walifanikiwa kumtambua mwanajeshi aliyehusika kumchukua Elie, ambae ni Luteni kanali Aaron Ndayishimiye, anayeongoza kikosi cha 212 kilichoko Rukoko, jirani na mpaka wa DRC, ambapo aliambatana na maofisa wengine wawili wa Serikali za mitaa ambao walimuonesha Elie alipokuwa.

Chama hicho kimesema kuwa tangu siku hiyo hawana taarifa zozote kuhusu mahali Elie Ngomirakiza alipelekwa, na kwamba wameviomba vyombo vya usalama kuchunguza mazingira ya kutekwa kwake.

Hata hivyo msemaji wa chama hicho, ameongeza kuwa walijaribu kumtafuta katika vituo vya polisi vilivyokaribu na eneo alikochukuliwa bila mafanikio na wanahofu kuwa huenda watekaji wakawa na lengo la kumuua.

Nae Rwasa, amesema kuwa licha ya kuingia kwa utawala mpya wa rais Evariste Ndayishimiye, wafuasi wa chama chake na viongozi wao bado wameendelea kufuatiliwa na vyombo vya usalama, akidai hata ofisi za chama chao kwenye maeneo mbalimbali ya nchi zimeendelea kushambuliwa.