WASOMAJI wetu wapenzi leo hii tunawaletea upishi mwanana wa Thariyd ambayo ni supu ya nyama kwa khubz Raqaaiq, upishi huu ni mzuri na inasemekana ulikuwa ukipendwa sana na Mtume Muhammad (SAW) na watu wengi wa Saudia Arabia.

Ili kuupika upishi huu ni lazima kuwa na mambo haya yafuatayo.

VIPIMO

Nyama ya mbuzi ya mifupa – 1 kilo

Kitunguu katakata vidogodogo sana – 3

Nyanya katakata ndogo ndogo au saga – 3

Thomu (saumu, garlic) ilosagwa – 1 kijiko cha kulia

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha kulia

Pilipili mbichi zisage – 2-3 takriban

Lumi (ndimu kavu) – 1

Hiliki ponda au saga – 3

Bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha chai

Nyanya paste (tomatoe paste) – 3 vijiko vya kulia

Ndimu au siki ukipenda – kiasi

Chumvi – kiasi

UKIPENDA ONGEZEA:

Viazi /mbatata menya katakata vipande – 2

Kusa (aina ya mumunya ya kijani madogodogo) – 3

Bilingani katakata – 1 la kiasi

Koli flower (cauliflower) katakata – ¼

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA   SUPU YA THARIYD

  1. Katika sufuria, weka nyama, hiliki, thomu, tangawizi mbichi, pilipili mbichi, bizari, chumvi, lumi. Weka katika moto ichemke hadi ikaribie kuiva na supu ibakie.
  2. Weka sufuria ndogo katika moto, kaanga vitungu hadi viwe laini na vigueuke rangi kidogo, tia nyanya kaanga, tia nyanya kopo kaanga.
  3. Mimina mchaganyiko wa nyanya katika supu.
  4. Mimina, viazi, na mboga zote acha ichemke kiasi, usiwivishe sana mpaka zikavurugika.
  5. Onja chumvi, ongezea ndimu au siku ukipenda. Tia hiliki na ongeza bizari ukipenda.
  6. Kabla ya kupakua, chota nyama na mboga weka upande.
  7. Katakata mikate ya raqaaiq katika sahani au chombo

8-Kisha mwagia supu irowane, kisha weka juu yake nyama .  Ukipenda weka supu ya nyama na mboga. Thariyd tayari….

VIDOKEZO: 

  1. Asili ya thariyd ni supu ya nyama na mikate tu, ila ukipenda kuongezea viazi na mboga kama karoti, koli flawa, bilingani, kusa vile upendavyo kama kwenye picha ifuatayo.
  2. Bonyeza upate upishi wa Khubz Raqaaiq
  3. Khubz raqaaiq huuzwa tayari kwa wingi katika bakeries au viduka vya kuchomwa mikate. Ikiwa hukupata unaweza kutumia mikate mingineyo.

Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)