NA GRACE GWAMAGOBE
UPUNGUFU wa watumishi katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa Mkoa wa Songwe, umepelekea mrundikano wa kesi hali inayoweza kusababisha ongezeko la uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Tebweta Mgumba, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda, alipofanya ziara ya siku mbili Mkoani hapa.
“Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Songwe inao watumishi wawili kati ya kumi wanaotakiwa kuwepo na hao wawili tu wanahudumia wilaya zote nne za Mkoa wetu, hawa lazima waelemewe na hivyo kupelekea kesi nyingi kuchelewa kukamilika, tunaomba mtutazame kwenye hilo.”, amesema Mgumba.
Ameongeza kuwa kuna changamoto ya ukosefu wa Mahakama za Wilaya ambapo kwa Mkoa wa Songwe ni Wilaya ya Mbozi pekee yenye mahakama huku Wilaya tatu zilizobaki zikitumia majengo ya kupangisha.
Mgumba pia amemueleza Naibu Waziri Pinda kuwa kuna ukosefu wa vifaa ikiwa ni pamoja na magari ambayo hutumika katika kusafirishia wafungwa pamoja na miundombinu ya maji katika magereza kutojitosheleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Mizengo Pinda, amesema kuhusu changamoto ya watumishi serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira, ili kuongeza idadi ya watumishi lakini Mkoa unapaswa kuangalia kesi ambazo sio za Msingi zifutwe ili kupunguza mrundikano wa kesi na mahabusu.
Naibu Waziri Pinda, ameongeza kuwa kesi nyingine zinaingiza hasara serikali kwani zinakuwa hazina msingi lakini pia kwa kesi ndogondogo mahakimu waangalie namna ya kutoa vifungo vya nje, ili kuipunguzia serikali mzigo wa kutunza wafungwa.