Na MWANAHAWA HARUNA
HALI ya usafi katika soko la Mwanakwerekwe imeimarishwa kutokana na kuwepo kwa vikundi vinavyofanya kazi hiyo, ikiwa ni hatua inayosaidia kuweka mazingira bora katika soko hilo.
Akizungumza na Zanzibar Leo, ofisini kwakwe Mwanakwerekwe, Mkuu wa Soko hilo, Juma Suleiman Juma, amesema hali ya usafi hivi sasa imefikia asilimia 90 ndani ya soko hilo, ambao unafanywa na vikundi vya usafi wakishirikiana wa wafanya biashara wa hapo.
Alisema mafanikio hayo yamefikiwa baada ya elimu kubwa waliyoitoa kwa wafanyabiasha wa hapo juu ya umuhimu wa kuweka safi sehemu za kufanyia biashara zao.
Alisema ndani ya soko hilo hivi sasa wameweka utaratibu maalumu wa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kufanya usafi ili kuzuiya kufanyabiashara hadi saa 3:00 asubuhi, ili kutoa nafasi kwao kufanya usafi huo.
“Wafanyabiashara katika soko letu sio wagumu wamekuwa wakishirikiana na sie kwa usafi wa pamoja katika soko kwa kusafisha maeneo yao ya kibiashara” alieleza.