NA SALUM VUAI

TATIZO la mazingira machafu na tabia ya wakaazi kutiririsha ovyo maji machafu katika shehia za wilaya ya Magharibi ‘B’, linaweza kusababisha janga iwapo juhudi za haraka hazitachukuliwa.

Utafiti uliofanywa mnamo mwezi Mei na Shirika la CCI (Centre for Community Initiatives) lenye makao makuu yake Dar es Salaam wilayani humo, umeonesha kuwa elimu juu ya uhifadhi wa taka na usafi wa mazingira bado haijawafikia wananchi ipasavyo.

Shirika hilo limejikita katika kutafuta changamoto za mitaa yenye ujenzi holela, ambayo kwa asilimia kubwa inakaliwa na watu wenye kipato cha chini, kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi kwa kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa.

Utafiti huo mdogo ulioandaliwa na CCI pamoja na Shirikisho la Miji Masikini Tanzania (TFUP), ulihusisha shehia tano za wilaya ya Magharibi ‘B’, ambazo ni Kinuni, Mwanakwerekwe, Muembe majogoo, Pangawe na Magogoni na kuonesha changamoto mbalimbali zinazohitaji kupewa kipaumbele katika kuzishughulikia.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa ZSSF Kariakoo mjini Zanzibar, Mhandisi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika shirika hilo Festo Dominick Makoba, alibainsha kuwa changamoto mbalimbali zimebainika lakini iliyo kubwa zaidi ni utupaji ovyo wa taka na maji machafu.

Alieleza kuwa, utiririshaji ovyo wa maji machafu unahitaji mamlaka husika kuweka miundombinu madhubuti na mifumo ya kisasa, badala ya kuwaachia wananchi wachimbe karo katika nyumba zao hata kama uchimbaji huo hauzingatii utaalamu.

Makoba alisema, sababu ya wakaazi wengi kutiririsha ovyo maji machafu, ni kuepusha karo za nyumba zao kujaa haraka, jambo alilosema linahitaji nguvu ya ziada kuielimisha jamii madhara yanayoweza kusababishwa na tabia hiyo, ambayo ni pamoja na kuibuka kwa maradhi ya mripuko.

Kuhusu tatizo la taka mitaani, alisema utafiti wao umebaini kukosekana kwa majaa rasmi katika maeneo mengi, na watu wamejenga utamaduni wa kutupa taka kwenye vichaka vya njiani wanapotoka majumbani asubuhi.