NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdallah Hussein Kombo, amesema kuwepo kwa tafiti za bahari kutasaidia kuimarisha uvuvi na nyezo za kusimamia zao la mwani.

Hatua hiyo pia itaufanya uvuvi kuwa endelevu na kuongeza thamani ya zao la mwani ili kuwanufaisha wakulima na wananchi kwa ujumla.

Kombo alitoa kauli wakati akizindua mukhtasari wa sera ya utafiti katika mazao ya bahari ambyo ni muhimu katika uchumi wa buluu uliotayarishwa na taasisi ya utafiti Tanzania COSTECH.

Alisema dhana ya uchumi wa buuu itafanikiwa kutokana na kuwepo kwa utafiti imara katika maeneo mbali mbali ikiwemo uvuvi, ukulima wa mwani na shughuli nyengine zinazofanywa na wananchi kwa kutumia bahari.

Aidha, Waziri Kombo alifahamisha kuwa, mbali ya kuzindua mukhtasari wa sera hiyo lakini utafiti huo unalenga kuongeza uzalishaji wa zao la mwani aina ya cotonii wenye bei kubwa pamoja na kushauri mbinu za kuongeza thamani wa zao la mwani.

Kombo aliishukuru taasisi ya COSTECH kusimamia tafiti zinazoendelea pamoja na mfuko wa maendeleo wa HDIF ya Uingereza kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha uchumi wa buluu ambalo ni eneo muhimu kwa ukuzaji wa uchumi wa Zanzibar.

Mapema kabla ya uzinduzi huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Mwita Mgeni Mwita, alisema serikali ya Zanzibar imekuwa ikisisitiza matumizi sahihi ya matokeo ya utafiti kama njia mojawapo ya kutatua changamoto zinazokabili maendeleo ya sekta za uchumi na ile zinazozorotesha maendeleo.

Alisema tafiti ndani ya idara ya mipango imekuwa ikiendelea vizuri pamoja na kushirikiana na taasisi nyengine za utafiti nchini zikiwemo ZARI, ZAHRI, Chuo Kikuu cha taifa Zanzibar (SUZA) na Idara inayosimamia utafiti katika kila wizara.

Akiwasilisha mada kuhusiana na hali halisi ya zao la mwani, Kamishana wa Idara ya Tume ya Utafiti Zanzibar, Dk. Afua Mohamed, alisema ipo haja ya kuwepo kichecheo cha kuongeza uzalishaji hususan mwani wa cottonii ili kumrahisishia mkulima wa zao hilo sambamba na kupata kipato kinachokidhi haja.