Kuanza kutolewa kwa wenye maradhi sugu, wanaohudumia watu wengi

NA HUSNA MOHAMMED

IKIWA leo Zanzibar inatarajiwa kupokea shehena ya chanjo za maradhi ya COVID -19 zilizokabidhiwa wiki iliyopita kwa niaba ya Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, mikakati kadhaa imeandaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar namna ya upokeaji, uhifadhi na utoaji wa chanjo hiyo kwa wananchi.

Chanjo hizo ambazo zilizotolewa na serikali ya Jamhuri ya watu wa China ikiwa ni kutimiza ahadi yake iliyoitoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa za Balozi wa Tanzania nchiniChina, Mbelwa Kairuki, akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, alisema amepokea chanjo hiyo aina ya Sinovac ambayo imeidhinishwa na shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha Balozi Kairuki aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huo ambao alisema utasaidia jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi hayo.

Hivyo alitoa rai kwa wananchi watakaopenda kuchanja kutumia fursa hiyo ya kujikinga na ugonjwa kwa kuchanja pamoja na kuchukua tahadhari zinazotolewa na wizara ya afya katika kujikinga na maradhi hayo.

Kairuki alisema msaada huo wa chanjo walizozipokea unatarajiwa kusafirishwa leo Julai 31 kutoka China mwaka huu na unatarajiwa kufika Zanzibar leo hii.

Wiki mbili zilizopita, balozi mdogo wa China Shang Shisceng, aliyepo Zanzibar, alikabidhi hati za msaada huo kwa makamu wa pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, ofisini kwake Vuga ili kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

MAFUNZO KABLA YA CHANJO

Gazeti hili limezungumza na mkuu wa kitengo cha kinga, Halima Ali Khamis, Mkuu wa Kitengo cha elimu ya Afya, alisema kuwa hivi sasa wizara ya afya kupitia kitengo cha kinga kiko katika harakati nyingi ikiwa ni pamoja na kuangalia tathmini namna ya utoaji wa chanjo hiyo kwa wananchi.

“Wakati wowote kuanzia sasa tutapokea chanjo kutoka China kwa sasa tunaandaa namna ya kuzihifadhi na utaratibu utakaotumika kwa wananchi wetu watakaokuwa tayari kuchanjwa”, alisema.

Hata hivyo, Halima alisema kuwa kwa kuanzia tayari chanjo hizo zimeanza kutolewa kwa wahudumu wa afya, wahudumu wa bandarini, wahudumu wa uwanja wa ndege na wale ambao kazi zao zinawafanya kukutana na watu wengi mara kwa mara.

Kuhusiana na mafunzo au taaluma kwa wananchi, Halima alisema kwa sasa wanakamilisha utaratibu wa kuwapa mafunzo wanahabari, viongozi wa dini, wanasiasa, watu wenye ulemavu, vijana, wenye maradhi sugu nakadhalika.

“Tumeona haja ya makundi haya kuwapa taaluma kwanza, lakini na wananchi ambao ndio kundi kubwa basi nao watapata taaluma kwa vyombo vya habari na watu waliokaribu nao kama viongozi wa dini”, alisema.

MAKUNDI YA AWALI YATAKAYOPEWA KIPAUMBELE

Halima aliyataja makundi ya kwanza ambayo yataguswa moja kwa moja na chanjo hizo kuwa ni pamoja na watu wenye maradhi sugu kama kisukari, ugonjwa wa moyo, saratani, wenye maradhi ya upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI), na maradhi mengine ambayo ni rahisi sana kuambukizwa corona.

“Tumeamua kuyalenga makundi haya kwa sababu yako katika uhatarishi mkubwa iwapo wataambukizwa corona kufariki mara moja”, alisema.

Sambamba na makundi hayo lakini pia Halima alisema kuwa wanakusudia kutoa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wanaohudumia watu wengi kama walimu wa skuli na madrasa, viongozi wa dini kwa maana misikiti na makanisa, mabenki, uwanja wa ndege, bandarini, mahospitalini nakadhalika.

UTAYARISHAJI WA UTOLEWAJI WA VYETI KWA WANAOCHANJA CORONA

Halima alisema kwa sasa wanaendelea na utaribu wa utoaji wa vyeti maalumu kwa wanaopatiwa chanjo.

“Tuko kwenye utaratibu wa  upatikanaji wa vyeti maalumu kwa wanaocanja ambapo kwa sasa bado hatujaanza labda kwa wanaosafiri nje ya nchi”, alisema.

Alisema utaratibu wote kwa hilo umekamilika na kwamba zoezi hilo baada ya kukamilika chanjo ya pili vyeti vitatolewa kwa waliochanja.

ASILIMIA 3 YA WANUFAIKA WA ZANZIBAR KUPATIWA CHANJO

Halima alisema kwa hatua ya awali watu wapatao asilimia 3 ya watu wa zanzibar watapatiwa chanjo hiyo.

“Watu wa Zanzibar wanakaribia milioni 2 hivyo kama asilimia tatu watapatiwa chanjo hiyo na baadae zitaendelea kutolewa.

WITO KWA WANANCHI

Mkuu huyo wa kitengo cha elimu ya afya aliwataka wananchi kuacha kudharau hasa palea ambapo serikali imeamua kutoa chanjo au zoezi lolote linalojali wananchi hasa kwa afya zao.

Alisema chanjo hiyo ni salama na wala haina tatizo lolote kwa kuwa imethibitishwa na shirika la afya duniani (WHO) huku nchi kadhaa ikiwemo china imeshaanza kutoa chanjo hiyo.

“Chanjo ni hiari anaetaka atachanja asietaka basi, haina haja ya kuleta kasumba zisizo kuwa na ukweli hapa zanzibar wapo watu wengi wameshachanja na hakuna tatizo lolote lililoripotiwa hadi sasa”, alisema.

Aliongeza kuwa, maradhi ya corona yapo zanzibar, tanzania na duniani kwa ujumla jamii inapaswa kufuata utaraibu wote uliotolewa na serikali na wataalamu wa afya kusudi kujikinga na ugonjwa huo.

Alisema uvaaji wa barakoa ni kinga kubwa dhidi ya maradhi ya upumuaji hasa hili la corona jambo ambalo litawakinga kupata maambukizi.

Hivi karibuni waziri wa afya, ustawi wa jamii, wazee, jinsia na watoto, nassor ahmed mazrui, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona ili kupunguza athari zake kama ilivyo katika mataifa mengine ulimwenguni.

Aliyasema hayo mara baada ya kupatiwa chanjo ya corona wakati wa zoezi la uzinduzi rasmi wa utoaji wa chanjo ya kwa ya awamu ya kwanza lililofanyika lumumba, mkoa wa mjini magharibi.

Alisema Zanzibar imethibitisha kesi zaidi ya sita za watu wanaougua ugonjwa huo hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kuchukua tahadhari kama zinavyotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kuvaa barakoa wanapokuwa kwenye misongamano.

Mazrui alisema, chanjo hiyo haina madhara yoyote kwa binadamu na kwamba imethibitishwa na shirika la afya ulimwenguni (W.H.O) ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya Zanzibar imeikubali.

Aliongeza kuwa pamoja na umuhimu wake, kuchanja ni jamo la hiyari hivyo kila anaetaka kufanya hivyo utaratibu utaandaliwa ili kupatiwa chanjo hiyo.

Hata hivyo, chanjo nyengine zinatarajiwa kuwasili leo kutoka China na kukabidhiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.