NA MWAJUMA JUMA

CHAMA cha Soka Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja (UWERFA), kimetoa adhabu ya kuzishusha madaraja mawili na faini ya shilingi 1,000,000, timu nne ambazo zimehusika na upangaji wa matokeo na utovu wa nidhamu.

Timu hizo ni Kundemba, Muungano Rangers, Umoja wa Mbuzini na New City ambazo mwakani zitashiriki ligi daraja la nne katika wilaya zao.

Hata hivyo licha ya kupewa  adhabu hiyo pia viongozi, wachezaji na waalimu ambao walikuwemo kwenye orodha katika michezo hiyo wamefungiwa mwaka mmoja na kupigwa faini ya shilingi 200,000 kila mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Msekwa Mohammed Ali, alisema adhabu hiyo wameitoa kwa mujibu wa kanuni na sio kumuonea mtu.

Alisema kwamba vitendo hivyo ambavyo wamevifanya wameharibu taswira nzima ya mpira wao wa Zanzibar.

Alifahamisha kwamba kamati tendaji ya UWERFA inakitafsiri kitendo hicho ni cha utovu wa nidhamu na walidharauliwa  na kuwatukana bila ya kujali uwepo wao.

Hata hivyo alisema kwa mtiririko wa maelezo hayo juu ya walichokishuhudia kamati ya mshindano na ripoti ya muamuzi na kamisaa wamegunduwa upangaji mkubwa wa matokeo wa kihstoria na utovu wa nidhamu wa wazi wa kutowaheshimu viongozi wa chama Cha mpira wa miguu Mkoani humo.

Alisema kwa mujibu wa kanuni sura ya 31 vitendo vyote vya utovu wa nidhamu vitakavyofanywa na timu, viongozi, wachezaji, wanachama, wapenzi, waamuzi na kamisaa na kusababisha nidhamu kuondoka ambavyo havikuelezwa katika kanuni hiyo kutaiwezesha ZFF kuchukuwa hatua za kinidhamu itazoona inafaa, kutegemea uzito wa kosa au tukio au kwa mujibu wa kanuni za CAF na FIFA.

Aidha alisema kwa mujibu wa kanuni sura ya 22 kifungu cha saba kinasema timu itakayoshiriki kwenye kupanga matokeo kwa tafsiri ya kanuni hiyo matokeo ya mchezo yatafutwa na hakutakuwa na timu itakayopewa pointi na timu hiyo itatozwa faini ya shilingi milioni moja ambayo itapaswa kulipwa si zaidi ya wiki moja.