NA KHAIRAT SULEIMAN (MCC)

VIJANA wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  wametakiwa kuacha chuki za wenyewe kwa wenyewe, ili kukisogeza mbele chama hicho.

Aliyasema hayo Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Shaaban Ali Othman, alipokua akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Wilaya ya Amani kichama uliofanyika katika Tawi la CCM kwa Wazee.

Alisema kuwa vijana wana kila sababu ya kukienzi Chama cha Mapinduzi kwa kudumisha amani na upendo baina yao kwani wao ndio tegemeo kubwa kwa chama hicho hata Taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwataka vijana hao kufuta dosari zao za nyuma na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo na kuepusha mizozo isiyo ya lazima.

Alisema ili kukiendeleza chama ni wajibu wao kugombania nafasi mbalimbali za uongozi na kutokata tamaa sambamba na kujitoa kwa uwezo wao wote kwa ajili ya Taifa.

Hata hivyo, alisema Taasisi ya vijana ndio inayowaandaa viongozi mbalimbali hivyo ni vyema kujitolea ili zinapotokea nafasi za ajira waweze kupewa kipaombele zaidi.

Alisema anathamini mchango wa vijana wa chama hicho na ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili ili kuondoa vijana tegemezi na ombaomba katika Wilaya hiyo.

Nae Mwenyekiti wa vijana Wilaya ya Amani Hassan Abdalla Said (Chaola) alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza siku 100 za uongozi wake.

Alimuomba Mwakilishi huyo kufikisha salamu kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya vijana zitumike ipasavyo, ili waweze kunufaika nazo.