NA ASIA MWALIM
JAMII imetakiwa kutumia kwa usahihi na kuwa na uelewa zaidi wa mitandao ya kijamii ili kuepuka kutoa taarifa zisizo sahihi na kwenda kinyume na sheria za nchi.
Msimamizi wa Mradi wa matumizi ya majukwaa ya kijamii na uhuru wa kujieleza unaotekelezwa na Zanzibar Youth Forum (ZYF), Almas Mohammed aliyasema hayo alipokua akifungua mafunzo ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hivi karibuni katika Kituo cha Walimu wa mkoa wa Kaskazini (TC), Mkwajuni Unguja.
Alisema vijana wengi wamejikita kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii hivyo wanapaswa kutambua sheria na matumizi yanayofaaa kwa kusambaza taarifa za kweli kwa jamii.
Katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha vijana na masheha wa mkoa huo, Almas alisema suala la upatikanaji habari ni nguzo ya msingi katika maendeleo ya mwanadaamu kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo watumiaji wanapaswa kutumia kwa uangalifu bila ya kwenda kinyume na sheria.
“Matumizi ya mitandao yamechukua nafasi kubwa zaidi kwa vijana, jambo ambalo linaendana na kasi ya maendeleo, hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia kutambua habari zinazofaa kusambazwa kwa jamii ili kuepusha madhara,” alieleza Mratibu huyo.
Aliongeza kuwa lengo jengine la mafunzo hayo ni kuinua uelewa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa kufuata sheria zinazoambatana na upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza.
“Moja ya mikakati ya kufikia malengo ya mradi huu ni kutoa elimu kwa makundi ya rika tofauti ili kuongeza utambuzi uliokusudiwa kwa jamii,” alieleza.
Akiwasilisha mada juu ya umuhimu na matumizi sahihi ya mitandao, Mkufunzi wa maswala ya habari, Ali nassor Sultan, alisema kutokana na utandawazi, mitandao ya jamii imechukua nafasi kubwa kwa kutoa habari na taarifa.