NA LAYLAT KHALFAN
OFISA Uhusiano, Habari, Masoko wa kitengo cha damu salama (Benki ya Damu), Ussi Bakar Mohammed, amesema vikosi vya SMZ vina mchango mkubwa wa kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.
Aliyasema hayo katika zoezi la uchangiaji damu katika Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU) Kilimani mjini Unguja.
Alisema vikosi hivyo ni wadau wakubwa katika uchangiaji damu kwa lengo la kuiwezesha serikali kuwa na damu ya kutosha ingawa kwa sasa kuna upungufu.
Asilimia 80 ya vikosi vya ulinzi ni wachangiaji wazuri wa damu salama katika kuokoa maisha ya watu hivyo tungependa muendelee ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa damu,” alisema.
Alisema zoezi hilo ni endelevu kwa vituo vyote vya unguja, hivyo aliviomba vikosi hivyo kuendeleza mashirikiano mazuri ya changiaji damu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, alifahamisha kuwa, lengo kuu la uchangiaji huo ni kuwasaidia wagonjwa pale wanaposhindwa kupata damu kwa haraka na kufanikisha kuokoa maisha yao.
“Ikitokezea kwa bahati mbaya mgonjwa hana damu mwilini ina maana hii ndio itakayowezesha kwa haraka kusaidiwa kwa mgonjwa huyo, hivyo tusiwe nyuma kuchangia huduma hii”, alisema.
Naye, Ofisa Utumishi kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU), ASF Ali Abdi Rashid, alisema kwa kuwa wanajua umuhimu wa maisha ya watu wanalazimika kuchangia damu kwa maslahi ya taifa.
“Tutakuwa bega kwa bega na benki ya damu ili kuona uhaba wa damu hapa nchini unaondoka kwani imetajwa kuwa ndio chanzo cha upatikanaji wa uhai wa watu kwani bila damu huwezi kuishi”, alisema ASF Ali.