HIVI karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifanya ziara ambayo ililenga kukagua miradi ya kijamii na ya kimaendeleo kwa mikoa mitatu ya Unguja.
Katika ziara hiyo aliyoanzia mkoa wa Kusini Unguja ambapo kwa siku mbili alikagua na kuitembelea miradi mbalimbali iliyomo kwenye wilaya ya Kusini na wilaya ya Kati zenye kuunda mkoa huo.
Alipomaliza ziara yake mkoa wa Kusini Unguja, akaelekea mkoa Kaskazini Unguja nako alifanya ziara kwa siku mbili akitembelea miradi katika wilaya za Kaskazini ‘B’ na wilaya Kaskazini ‘B’.
Ziara hiyo ilihitimishwa katika mkoa wa Mjini Magharib, ambapo alitembelea na kukagua miradi katika wilaya tatu, za Maghabi ‘A’, Magharib ‘B’ na wilaya ya Mjini.
Tuseme tu ilikuwa ziara muhimu sana kwa Dk. Mwinyi na kiukweli aliifanya katika wakati mufaka, hasa ikizingatiwa kuwa imempa uelewa na ufahamu mkubwa wa mambo yalivyo katika jamii.Uzuri wa ziara hiyo ni kwamba rais aliwapa nafasi wananchi katika maeneo yote aliyoyafikia ambapo bila ya woga wananchi hao walieleza shida, kero na changamoto zinazowakabili hasa za ukosefu wa upatikanaji wa huduma za jamii.
Wapo wananchi waliowasilisha kwa Dk. Mwinyi shida ya upatikanaji wa huduma ya maji safi, wapo walielezea shida ya barabara, wapo walioelezea changamoto ya ya uhaba wamadarasa, wengine hawana umeme nakadhalika.
Mfumo huu uliofanywa na Dk. Mwinyi wa kuwapa nafasi wananchi kuzungumza kero zao katika ziara hiyo una umuhimu mkubwa, kwani unatoa nafasi ya kuonesha kiwango cha uwajibikaji wa wateule wake na uwezo wao katika kuzitatua changamto za jamii.
Ingawaje rais mwenye amejionea katika ziara yake hiyo, sisi tunaamini kwamba baadhi ya changamoto zilizobainishwa na wananchi wala hazikupaswa kuwasilishwa katika ziara ya rais.
Ni changamoto ambazo zilihitaji maarifa na uwezo wa kiungozi katika kutatuka kwake na sio mpango makakati ambao pengine ungemfanya mteule arudi ofisini akauandae au bajeti ya mabilioni apatiwe kutoka hazina.