NA HUSNA MOHAMMED

BADO Zanzibar inaendelea kuandamwa na janga la vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia licha ya hapo jana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kukutana na wadau wa vitendo hivyo.

Mara kadhaa kumekuwa na malalamiko kuhusiana na kesi za udhalilishaji ambapo imekuwa kama ni kitu cha kawaida katika jamii zetu.

Nasema hivyo kwa kuwa hakuna hata siku moja ambayo hakuripotiwi kesi za aina hiyo katika vyombo vya habari jambo ambalo linaitia aibu visiwa vyetu.

Na cha kushangaza utakuta kesi za namna hii huripotiwa kwa watu wa karibu sana na ndio maana kufikia mwisho mzuri ni vigumu sana kwa jamii na familia kuchelea muhali.

Kwa mujibu wa ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali Zanzibar ilitoa takwimu ya kesi za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ambapo ilisema watu 571 wamebakwa Unguja na Pemba wakiwa miongoni mwa waathirika wa matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia mwaka 2020.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa miongoni mwa waliobakwa walikuwa wanawake 64 na wasichana 507, waliolawitiwa ni 102, kiingiliwa kinyume na maumbile 46 ambao mwanamke ni mmoja na wasichana 45.

Hata hivyo, mlinganisho wa mwaka 2019 na 2020, umepungua kutoka matukio ya kubaka 651 hadi 571, kulawiti matukio 157 hadi 102.

Kiujumla wake takwimu zinaonesha jumla ya matukio 1,363 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwaka 2020 ambapo wanawake na watoto wamekuwa waathirika wakuu.

Aidha waathirika 217 walikuwa wanawake sawa na asilimia 15.9 na watoto 1,146 sawa na asilimia 84.1,  miongoni mwao wasichana 899 (asilimia 78.4) na wavulana walikuwa 247(asilimia 21.6).

Wilaya ya Mjini imeelezwa ndiyo iliyoshika nafasi ya kwanza ikiwa na matukio 297, ikifuatiwa na Magharibi ‘B’, matukio  273 na Micheweni ikiwa na idadi ndogo ya matukio 41.

Hata hivyo, idadi ya matukio  kwa mwaka uliopita  imepungua kidogo kwa asilimia 0.4 kutoka matukio  1,369  mwaka 2019 hadi 1,363 maka 2020.

Sambamba na hilo, lakini watoto wenye umri wa miaka 15-17 wameripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio 681 sawa na asilimia 59.4 ya matukio yote ya watoto ni zaidi ya robo mbili ukilinganisha na miaka mengine ya watoto.

Matukio mengi yameonesha kutokea majumbani yakiwa ni 1,270 sawa na asilimia 93.2, ikifuatiwa na sehemu neyngine ikiwemo kazini, skuli na madrasa kiasi kwamba inaonesha Dhahiri kuwa watendaji wa matukio hayo ni watu wa karibu sana.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa udhalilishaji wa kijnsia dhidi ya wanawake na watoto utaendelea hasa baada ya baadhi ya watu, askari, watendaji na wahanga wa matukio hayo kujifanya wasuluhishi na hivyo kesi hizo kumalizika kinyemela.

Panapoamulika kuzisuluhisha kesi hizo majumbani, vituo vya polisi, kwenye taasisi za kidini au kwengineko ni wazi kuwa tunawajengea mazingira mazuri watendaji wa mambo hayo.

Hivyo basi ipo haja ya kujiuliza ni kwa nini umsamehe mtendaji wa makosa hayo ilhali amemuharibia mtoto mustakbali mzima wa maisha yake yote?.

Ni kwanini asionewe huruma yule aliyetendewa ukatili hasa ikizingatiwa kuwa ameharibika kisaikolojia na badala yake mtendaji aliekuwa hakupata athari yoyote aendelee na maisha mazuri.