NA MWAJUMA JUMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya salum, amesema Ofisi yake inathamini mchango unaotolewa na waandishi wa habari katika mapambano dhidi ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
Alisema kuwa waandishi wa habari ni wadau muhimu katika vita hiyo kwani wao ndio daraja la kufikia mafanikio kwenye kupambana na vitendo vya uuzaji, usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wa kuwatoa vijana walioteleza ili wawe vijana bora.
Dk. Mkuya aliyasema hayo wakati wa bonaza la michezo la kuadhimisha wiki ya kupiga vita usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya lililofanyika viwanja vya Mao Zedong, Mjini Unguja, lililoandaliwa na tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar.
Alisema kuwa kitendo cha kuwakusanyisha waandishi wa habari na makundi mengine ya jamii ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe wa mapambano hayo.
“Nawapongezeni sana waandishi wa habari sio kwa sababu leo mmeshinda bali pia ni kutokana na kwamba mmetusaidia sana katika kufikisha ujumbe kwa vijana na wananchi wenzetu,” alisema Dk. Mkuya.