NA HAFSA GOLO

ZAIDI ya shilingi milioni 50 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kisasa katika jimbo la Donge, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza na wananchi na viongozi wa jimbo hilo, Mwakilishi wa jimbo hilo Dk. Khalid Salum Mohamed mara baada ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya ujenzi wa miradi ya maendeleo vilivyogharimu zaidi ya shilingi milioni 5.

Alisema lengo la ujenzi wa hospitali hiyo ni kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuimarika na huduma zote za kinamama zinapatikana ipasavyo.

Aidha alisema utekelezaji wa ujenzi huo ni miongoni mwa ahadi zao kwa wananchi wakati wakiomba nafasi ya kuliongoza jimbo hilo katika uchaguzi mkuu.

“Tunaendelea kushirikiana kwa pamoja kutimiza ahadi zetu, utatuzi wa kero za wananchi na ujenzi za miradi ya maendeleo,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo jimboni humo inakamilika kwa wakati, wataendelea kuwashajihisha wadau wa maendeleo pamoja na serikali kuongeza nguvu pale itapohitajika.

Aliwasisisitiza wananchi kudumisha utamaduni wa kujitolea katika ujenzi wa taifa kwani itasaidia kuongeza ari na kuleta ufanisi wa maendeleo jimboni humo,” alisema.

Nae Mbunge wa Jimbo hilo, Soud Mohamed Juma alisema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa hospitali viongozi hao watasimamia masuala ya kilimo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa trekta.

Alisema viongozi wanatambua kwamba wananchi wengi wa jimbo hilo wanajishughulisha na masuala ya kilimo hivyo miongoni mwa vipaumbele vyo ni kuona wakulima wanapata pembejeo na huduma muhimu za kilimo.“Tumedhamiria wakulima wetu jimboni humo mnapiga hatua na kilimo kinawakomboa na umasikini,” alisema.