NA ASIA MWALIM

WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kutumia mitandao ya kijamii kuwa chanzo cha utatuzi wa migogoro badala ya kuchochea maafa yanayotokea kwenye jamii.

Ushauri huo umetolewa na Mwandishi wa habari muandamizi ambae pia ni Mkufunzi Suleiman Seif Omar, alipokua akitoa mafunzo ya matumizi sahihi ya mitandao kwa waandishi wa habari na vijana wa taasisi mbalimbali huko Kidongo chekundu Zanzibar.

Alisema waandishi wa habari wanatakiwa kuendana na wakati na kutumia mitandao ya kijamii katika kufikisha taarifa zinazohamisha vitu vya msingi ikwemo maendeleo na amani ya nchi.

Aidha alisema baadhi ya waandishi wanatumia mitandao vibaya kwa kukosa utafiti wa vitu wanavyo viwasilisha katika jamii na kuandika uongo, jambo ambalo ni kinyume na maadili yao.

Mapema Mkufunzi huyo alieleza kuwa kila nchi inaongozwa na mipaka yake, hivo jamii itumie uhuru wa mitandao uliopo, katika kutoa maoni na kupokea taarifa bila ya kuathiri sheria za nchi.

“Kuna watu hutumia mitandao kwa kumchafua mtu au kiongozi, bila ya kujua kua ana kwenda kinyume na sheria ya nchi yetu” alisema.

Alieleza kuwa licha ya uhuru huo maudhui yanayopaswa kutolewa na kupokelewa yaendane na utaratibu wa nchi husika, hivyo alishauri waandishi wa habari na vijana kusambaza ujumbe kama maadili ya habari yanavyotakiwa.

“Tumeshushudia katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu husambaza picha, video na ujumbe ambazo hazina maadili ya habari na mara nyengine kuhatarisha amani ya nchi” alisema.

Akizungumzia haja ya kutoa mafunzo hayo, alisema kutokana na ukubwa wa matumizi ya mitanadao unavyoendelea kukua kwa kasi ni muda muhimu wa kutoa mafunzo hayo, ili kuiendekeza amani na utulivu uliopo nchini.

Alisema vijana ni watumizi wakubwa wa mitandao, uwekaji taarifa katika mitandao inakuwa njia rahisi pia kupata wasomaji wengi kwa wakati mchache kuliko vyombo vyengine vya habari.

Alisema kuna mitandao mingi ya kijamii muandishi anapaswa kutumia kuweka habari zake na matukio mbalimbali yanayoendelea, kitu cha msingi kuzingatia ni kufanya utafiti wa kina na kusoma sheria za mitandao ili kuwasaidia.

Mrajisi Tume ya Utangazaji Zanzibar, Sheikha Haji Dau, alisema mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuweka na kuvunja amani kwa kutumia mipaka, hivyo alisisitiza kutoa habari kwa kuzingatia sheria, sera na kanuni husika.

Alisema licha ya Tume hiyo kutoa maelekezo kuhusiana na matumizi sahihi ya mitandao ikwemo ukataji wa leseni, bado kuna changamoto ya watu wengi kukosa kuasjili kisheria jambo ambalo linahatarisha usalama.

Alifahamisha kuwa waandishi na vijana mbalimbali wanapotumia mitandao ya kijamii waogeze wigo katika akili zao kwa kujua mambo mengi kwa haraka hivyo ni wakati wa kuelekeza nguvu zao katika mitandao bila ya kuathiri sheria ya nchi na kukiuka maadili.

Alisema vijana wana nafasi kubwa katika jamii, na kudhibiti ni jambo zuri hivyo muongozo huo umekusudia kulinda na kuendeleza amani ya nchi iliopo wakati huu.