NA LAYLAT KHALFAN

MHARIRI Mtendaji wa Shirika la Magazeti Zanzibar, Yussuf Khamis, amewasisitiza waandishi wa Habari wa shirika hilo, kuwa na utamaduni wa kujifunza pale furasa zinapojitokeza ili kujijengea mustakbali mzuri wa kazi zao za kila siku.

Aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya sera ya jinsia kwa vyombo vya habari, yaliyofanyika katika ofisi za shirika hilo, Maisara Zanzibar.

Alisema waandishi wa habari wengi wa Zanzibar wana viwango vidogo vya elimu kutokana na kushindwa kujiongezea elimu kutokana na sababu mbali mbali.

Aidha, alifahamisha kuwa ili kuepukana na hali hiyo ni vyema watilie mkazo masuala ya kujifunza ili kuimarisha ukuaji wa elimu badala ya kuridhika na walipopata.

“Bila ya kujifunza kamwe huwezi kufika mahala na wengi wao wanaoendelea na kufanikiwa ni wale wanaopenda kujiendeleza kupitia mafunzo mbali mbali rasmi na yasiyo rasmi”, alisema Yussuf.

Akiwasilisha mada kuhusiana na sera ya kijinsia kwa vyombo vya habari, mwandishi mwandamizi na mshauri wa vyombo vya habari, Hawra Shamte, aliwanasihi waandishi wa habari wasiridhike na uandishi wa habari na badala yake wajitolee na kujikita katika mambo mbalimbali yenye tija kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kujitengenezea mazingira bora katika vyombo vya habari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza ndani ya vyombo vya habari ikiwemo ukatili na ukandamizaji wa kijinsia.

“Sera imebainisha na kutaka vyombo kuweka mkakati wa kuimarisha usawa wa koijinsia sio katika watendaji tu, bali hata habari zinazoandikwa na vyanzo vinavyotumika katika habari,” alieleza Hawra.